HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 9 November 2017

COSTECH KUTUNGA SHERIA ITAKAYOSIMAMIA MASUALA YA UTAFITI NCHINI

 Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dugushilu Mafunda akizungumzia namna taasisi yao ilivyoweza kusimamia tafiti mbalimbali na kushindwa kufanyiwa kazi ikiwa ni siku ya mwisho ya maadhimisho ya miaka 40 ya ushirikiano wa masuala ya utafiti baina ya Tanzania na Sweden leo Jijini Dar es Salaam.

                                   Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeweka mapendekezo matano ya tafiti sambamba na kutunga sheria zitakazowapa muongozo watafiti pindi wanapotaka kufanya utafiti wa aina mbalimbali.

Akizungumza leo katika siku ya mwisho ya maadhimisho ya miaka 40 ya ushirikiano wa utafiti baina ya Tanzania na Sweden yaliyoanza jana, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dugushilu Mafunda amesema kuwa kwa sasa wamejikita katika mapendekezo matano ambayo yamegawanyika katika vipengele mbalimbali ambapo kupitia taasisi yao wanafanya tafiti hizo.

Mafunda amesema kuwa, kuna tafiti nyingi sana zimeshafanyika ila zinashindwa kufanyiwa kazi kutokana na baadhi ya tafiti hizo kuhitaji miradi mikubwa kwenye kuiendesha. 
"Tafiti nyingi tayari zimeshafanywa na kikubwa zaidi zaidi zimekuwa zinashindwa kuendelea kufanyiwa kazi kutokana na baadhi ya tafiti hizo kuhitaji miradi mikubwa ya uendeshaji, zaidi ni makampuni ya kujitokeza kwa ajili ya kusaidia kufanyika,"amesema Mafunda.

COSTECH wamekuwa mstari wa mbele katika kusimamia tafiti mbalimbali zinazoendeshwa nchini huku wakiwa kwenye hatua za mwisho za kutunga sheria zitakazokuwa zinawataka watafiti kufuata maadili kwenye tafiti zao.

Akieleza hayo Afisa mwandamizi wa Utafiti (COSTECH) Hildegalda Mushi amesema kuwa kuna taasisi nyingi kwa sasa zinafanya tafiti kwenye nyanja tofauti ila tumeamua kutunga muongozo huu kwa ajili ya kusaidia kusimamia maadili bora.

"Muongozo huu ambao utakamilika Januari 2018 utaweza kusimamia ubora kwenye kulinda mazingira ya binadamu, wanyama na mifugo pia tafiti hizo zitakuwa kwa matakwa ya kitaifa na kimataifa,"amesema Hildegalda.

Amesema tafiti zote haziwezi kufanyika mpaka waweze kupata kibali na iwapo mtafiti ataenda kinyume na muongozo basi atakumbana na adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kibali cha kufanya tafiti au kuondolewa kabisa kwenye masuala ya utafiti.

Kwa upande wa Mhadhiri wa chuo cha Ardhi Prof Nancy Marobhe ambaye amefanya tafiti inayohusu masuala ya usafishaji maji kwa njia ya kutumia mbegu ambayo aliifanya mwaka 2008 Singida vijijini.

Prof Nancy amesema kuwa, aliweza kufanya tafiti hiyo katika vijiji vitano na aliweza kukutana na changamoto kubwa wanazokutana nazo wakina mama wakati wa upatikanaji wa maji safi na salama na kwenda kuishia kuchota maji kwenye marambo (mabwawa) na maji hayo wakiyasafisha kwa kutumia mbegu za asili za mlonge na mkeketa.

Tayari ameweza kutoa njia nzuri ya kuwasaidia wanawake kuweza kusafisha maji kwa njia ya mbegu na wataweza kufanya hivyo ikiwa ni salama zaidi na watatumia unga wa mlonge na mkeketa kwa kiasi kidogo sana.

Changamoto kubwa ni kuwa upatakinaji wa maji kwa vijijini umekuwa mdogo sana kwani visima vingi vinavyojengwa vinakuwa havifanyi kazi kutokana na baadhi ya watu kushindwa kuvitunza na wengine kuviharibu.


Afisa mwandamizi wa Utafiti (COSTECH) Hildegalda Mushi  akielezea muongozo wa sheria utakaosimamia tafiti mbalimbali ambapo utakamilika Januari 2008 ukiwa na matakwa ya kitaifa na kimataifa. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Utafiti (COSTECH) Dr Khadija Malima wakati wa siku ya mwisho ya maadhimisho ya miaka 40 ya ushirikiano wa masuala ya utafiti baina ya Tanzania na Sweden.

 Mhadhiri wa chuo cha Ardhi Prof Nancy Marobhe akizungumzia tafiti yake aliyoifanya mwaka 2008 
inayohusu masuala ya usafishaji maji kwa njia ya kutumia mbegu 
 wakati wa siku ya mwisho ya maadhimisho ya miaka 40 ya ushirikiano wa masuala ya utafiti baina ya Tanzania na Sweden.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad