HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 9, 2017

NEC YASAMBAZA VIFAA VYA UCHAGUZI

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa maandalizi ya vifaa kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani unaofanyika katika kata 43 yamekamilika na awamu ya pili ya vifaa vitaanza kusafirishwa leo Ijumaa kwenda katika kata husika.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Kailima Ramadhani, alisema kwamba vifaa vitakavyosafirishwa kuanzia kesho ni maalumu kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa vituo, makarani waongozaji pamoja na  mfano wa karatasi za kupigia kura.

Alisema awamu ya kwanza ya kusafirisha vifaa ulifanywa na tume wakati wa mafunzo ya wasimamizi wa uchaguzi ambayo yalifanyika mjini Dodoma ambavyo vilitumika wakati wa uteuizi wa wagombea udiwani katika kata zote.

“Napenda kuwahakikishia umma kwamba tume imejipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi huu na maandalizi ya kupeleka vifaa katika husika yako vizuri na awamu ya pili ya upelekaji wa vifaa itapaelekwa kesho (leo),”alisema Ramadhani.

Alisema awamu ya tatu ya usafirishaji wa vifaa itahusisha  vifaa vichache ambavyo ni karatasi za kupigia kura pamoja na fomu za kutangazia washindi ngazi ya kituo na ngazi ya kata.

Naye Mkurugenzi wa Manunuzi, Ugavi na Logistiki wa NEC Eliud Njaila, alisema kwamba NEC imepeleka vifaa vya kutosha katika vituo vyote 893  vilivyoko katika kata 43 na hakutakuwa na upungufu wowote.

Alisema kwamba katika awamu ya pili ya upelekaji wa vifaa, wameweka na mfano wa karatasi za kupigia kura ili wadau ambavyo ni vyama vya siasa vijiridhishe kuhusu karatasi hivyo zitakavyokuwa pamoja na kufanya uhakiki wa majina wa wagombea wao.

“Tunaamini kwamba vyama vya siasa vitahakiki majina ya wagombea wao kwa kila kata ili kama kuna masahihisho wayalete mapema na NEC iweze kufanya masahihisho haraka wakati wa kuchapa karatasi halisi za kupigia kura,” alisema Njaila.

Njaila pia aliwataka wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya kuwatumia maafisa boharia katika kupokea na kutunza vifaa hivyo. Alisema wataalamu hao pia ndio watumike pia kusafirisha vifaa hivyo kwa kuwa wao wana ujuzi wa namna ya kutunza na kugawa vifaa.

Aliongeza kuwa iwapo wasimamizi wa uchaguzi watawatumia maafisa ugavi ni wazi kuwa hakutakuwa na malalamiko ya kupungua kwa vifaa katika vituo vya kupigia kura.

 Naye Ofisa Uchaguzi wa NEC Sada Kangeta, alisema kuwa tayari wameshafanya uhakiki wa vifaa vya uchaguzi na wamejiridhisha kuwa vifaa vyote vipo kama inavyopaswa na kwamba hatua itakayofuata ni usafirishaji wa vifaa hivyo katika maeneo husika.

Aidha aliwataka wapiga kura wote wa maeneo husika, wagombea wa vyama vyote vya siasa na wadau wa siasa kutokuwa na hofu juu ya vifaa hivyo kwa madai kuwa hakuna upungufu wowote utakaojitokeza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad