HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 30 August 2017

ZIARA YA KAMISHNA WA MADINI MKOANI GEITA

Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (wa pili kutoka kushoto), akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa Huduma za Jamii wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Manase Ndoroma (wa kwanza kushoto). Wengine ni maofisa kutoka wizarani na GGM.
Na Veronica Simba – Geita

Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, amefanya ziara katika Mkoa wa Geita, ambapo ametembelea maeneo mbalimbali ukiwemo Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Kijiji cha Nyakabale, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo.

Ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake rasmi ya kikazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kamishna Mchwampaka, jana, Agosti 29, alifanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu, Ezekiel Kyunga, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Selestine Gesimba na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi ambapo walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika kusimamia shughuli za sekta ya madini kwa manufaa ya wananchi wa Geita na Taifa zima.

Akiwa katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Kamishna Mchwampaka ambaye alifuatana na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria-Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba, Afisa Madini wa Mkoa wa Geita Ali Said Ali na maafisa wengine kutoka wizarani, alipokea taarifa ya utendaji kazi wa Mgodi huo na kukagua maeneo na shughuli mbalimbali zinazofanyika mgodini.

Aliwataka watendaji na viongozi wa Mgodi kuendelea kuimarisha mahusiano na jamii inayowazunguka ili kuondoa migogoro iliyopo na kuepusha migogoro mingine kujitokeza.

Akizungumza na viongozi wa Kijiji cha Nyakabale, Benard Kazuri (Mtendaji) na Ndalahwa Elias (Mwenyekiti), aliwataka kuwaelimisha wananchi wao kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi, hususan zinazohusu masuala ya madini kwa kuachana na tabia ya uvamizi na kuiba katika Migodi ya wawekezaji wakubwa badala yake waendelee kujiunga na vikundi mbalimbali vya uchimbaji mdogo na kuendesha shughuli hizo kwa kufuata taratibu husika ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (wa tatu kutoka kulia), akikagua moja ya maeneo kunakofanyika uchenjuaji wa dhahabu za wachimbaji wadogo katika kijiji cha Nyakabale wilayani Geita.
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka na timu yake wakikagua Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), katika shimo la wazi (Open pit).
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (katikati), akikagua sehemu ya chini (underground) ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM). Pamoja naye ni maofisa kutoka wizarani na GGM.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Meja Jenerali mstaafu, Ezekiel Kyuga (kushoto), akizungumza na Kamishna wa Madini na Timu yake, walipofika kumtembelea ofisini kwake.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad