HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 14, 2017

Waziri Mpango awasimamisha kazi watumishi wanne wa TRA

Na Benny Mwaipaja, Songwe/Mbeya 
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewasimamisha kazi watumishi wanne wa Idara ya Forodha, katika Mpaka wa Tanzania na Zambia, Mjini Tunduma, ili kupisha uchunguzi wa kudaiwa kuhusika na upotevu wa lakiri 10 zinazotumika kufunga kwenye shehena ya mizigo inayopita mpakati hapo kutoka nje ya nchi.

Mpango amewataja watumishi hao kuwa ni pamoja na Harrison Mwampashi, John Makorere, Stephene Josia na Frank Kessy na kuviagiza vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama mpakani hapo viwahoji huku wakiwa wamesimamishwa kazi.

Watumishi hao wanadaiwa kuiba lakiri hizo kumi kutoka ofisi za TRA-Tunduma wanakofanyiakazi, ambapo 4 kati ya hizo lakiri zilikutwa zimefungwa kwenye mizigo ya malori yanayoshikiliwa katika mpaka huo baada ya uchunguzi kufanyika huku malori mengine 5 yakizuiwa baada ya kuonekana lakiri zao zimechezewa.

Taarifa zinasema kuwa baada ya uchunguzi, mawakala ama wamiliki wa malori hayo wamedai walipewa lakiri hizo na watuhumiwa na kwamba uchunguzi zaidi umebaini kuwa kiwango cha mizigo kilichomo kwenye makontena yaliyobeba mizigo ya magogo na kufungwa lakiri hizo za wizi hakilingani na idadi ya
mizigo iliyoko kwenye nyaraka jambo linaloashiria kuwa wanazitumia lakiri hizo kudanganya idadi na uzito wa mizigo yao ili kukwepa ushuru na kodi mbalimbali za Serikali.

“Hakuna kitu muhimu kama uadilifu kwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato na hatutasita wala hatutamwonei aibu mtu yeyote, tutachukua hatua kwa mujibu wa sheria ili kulinda fedha za umma,” alionya Dkt. Mpango.

Alisema kuwa Serikali imebaini baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato na Idara za Forodha mipakani wanashirikiana na wafanyabishara wasio waaminifu kuingilia mifumo ya kukusanyia mapato, kitendo ambacho kinaweza kurudisha nyuma juhudi za serikali kuwahudumia wananchi wake.

Dkt. Mpango amewaonya wafanyakazi wote wa forodha na Mamlaka ya Mapato nchini, kuwa wazalendo na waaminifu katika kukusanya mapato ya Serikali na kuacha kujihusisha na vitendo vinavyokwaza ufanisi wa Mamlaka hayo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad