1. Hivi
karibuni kumekuwa na takwimu zinazotolewa na Kampuni ya GeoPoll yenye Ofisi ya
Kanda ya Afrika Mjini, Nairobi Kenya. Takwimu hizo ambazo hutolewa kwa njia ya
mitandao ya kijamii, zinahusu ukusanyaji wa taarifa za Televisheni na Redio
nchini kwa idadi ya watazamaji na zinatolewa kila baada ya miezi mitatu.
2. Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) inapenda kuujulisha umma kuwa takwimu hizo sio Takwimu
Rasmi (Official Statistics) kwa kuwa hukusanywa kwa mfumo ambao hautambuliwi na
NBS kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.
3. Takwimu
Rasmi kama ilivyofafanuliwa katika kifungu cha 20 cha Sheria ya Takwimu ni
takwimu ambazo zimetolewa kwa kufuata Misingi ya utoaji Takwimu Rasmi
(Fundamental Principles of Official Statistics) na utolewaji wake umeratibiwa
na NBS. Hivyo basi, takwimu zinazotolewa na taasisi au mtu yeyote zitatambuliwa kuwa Takwimu Rasmi
iwapo tu zitakidhi vigezo vinavyotolewa
na kusimamiwa na NBS.
4. Kwa
mantiki hiyo, takwimu zinazotolewa na mtu au taasisi yoyote bila kufuata au kukidhi vigezo vinavyotolewa
na NBS kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu, hazitambuliwi kuwa ni Takwimu Rasmi na
kwa maana hiyo haziwezi kutumika katika
kupanga mipango ya maendeleo ya nchi.
5. NBS
inaitaka Kampuni ya GeoPoll kufuata taratibu zilizoainishwa katika Sheria ya
Takwimu, kwa kuwa takwimu zinazotolewa na kampuni hiyo hazijakidhi vigezo vya Takwimu
Rasmi na zinapotosha umma na kuleta
mkanganyiko kwa wadau pamoja na
kuathiri mahusiano ya kiutendaji baina ya vyombo
vya habari hapa nchini.
Kuhusu Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya
Takwimu ya Mwaka 2015. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, NBS imepewa mamlaka ya kutoa,
kusimamia na kuratibu upatikanaji wa takwimu rasmi kwa ajili ya matumizi ya
Serikali na wadau wa takwimu.
Aidha,
kifungu cha 6 cha Sheria hiyo ya takwimu, kinaipa NBS jukumu la kutoa na
kusimamia Miongozo na Viwango vya utoaji wa Takwimu Rasmi.
Imetolewa na: Mkurugenzi Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS), Dar es Salaam.
07 Agosti, 2017.
No comments:
Post a Comment