HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 25, 2017

EA YAKAMILISHA UKARABATI WA SHULE 10 KONGWE ZA SERIKALI.

 Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Sylvia Lupembe (kulia) akiongea na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na kukamilika kwa ukarabati wa shule kongwe 10 za Serikali. Kushoto ni Meneja Ufadhili Miradi ya Elimu, Anne Mlimuka.
Meneja Ufadhili Miradi ya Elimu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Anne Mlimuka akiongea na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na malengo ya mradi wa ukarabati wa shule kongwe 10 za Serikali. Kulia ni Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa TEA, Sylvia Lupembe. (Picha na Fatma Salum-MAELEZO)

 TNa. Neema Mathias-MAELEZO
MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imekamilisha awamu ya kwanza ya ukarabati wa shule 10 kongwe za Serikali ili kusaidia kuwepo kwa miundombinu bora ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuongeza nafasi za wanafunzi kupata elimu.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa mamlaka hiyo Bi. Sylvia Lupembe wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na  maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa Shule Kongwe za Sekondari, ambao  unatekelezwa na Serikali kupitia TEA na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na wadau wengine.

“TEA inakarabati takriban shule kongwe 17 kati ya 87 na tumeanza ukarabati wa shule 10 katika awamu ya kwanza unaogharimu shilingi bilioni 10, mpaka sasa ukarabati huo umefikia asilimia 80 na ifikapo mwezi Oktoba utakuwa umekamilika. Shule nyingine 7 zitakarabatiwa katika awamu ya pili,” alifafanua Bi. Lupembe.

Alizitaja shule zinazokarabatiwa kuwa ni Mzumbe na Kilakala - Morogoro, Shule ya Sekondari ya wasichana Msalato-Dodoma, Shule ya Sekondari Mwenge - Singida, Shule ya Sekondari Pugu - Dar es Salaam, Shule ya Sekondari Ilboru –Arusha, Shule ya Sekondari Same-Kilimanjaro, Shule ya Sekondari Tabora Wavulana na Tabora Wasichana na Shule ya Sekondari ya Wasichana Nganza iliyopo Mwanza.

Aidha Bi. Lupembe aliongeza kuwa awamu ya kwanza ya ukarabati umehusisha miundombinu ya majengo ikiwemo mabweni, madarasa, majengo ya utawala, kuboresha mifumo ya maji safi na maji taka, mifumo ya umeme pamoja na mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

“Tayari makabidhiano ya awali yamefanyika kwa baadhi ya majengo hususan mabweni na madarasa katika shule za Msalato, Mwenge na Mzumbe,” alieleza Bi. Lupembe.
Bi. Lupembe alibainisha kuwa mafanikio kutokana na mradi huo yameanza kuonekana kwani ari ya wanafunzi kusoma imeongezeka na idadi ya usajili wa wanafunzi imeongezeka katika shule ya Mwenge na nyingine zilizokarabatiwa.

Kwa upande wake Meneja Ufadhili Miradi ya Elimu Bi. Anne Mlimuka alieleza malengo mbalimbali ya mradi huo ikiwa ni pamoja na kuhifadhi ubora wa miundombinu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora katika mazingira bora, kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi katika shule za Serikali na kuboresha miundombinu ya maabara kwaajili ya wanafunzi wa masomo ya Sayansi ili kuendana na Sera ya Viwanda inayohitaji wataalam wengi wa Sayansi.

“Mradi huu wa kukarabati shule kongwe utakapokamilika utaendelea kwenye shule za Kata ili kuirudisha elimu katika hadhi yake na kuzifanya shule zote za serikali nchini zitoe elimu bora, wataalam bora katika mazingira bora kama ilivyokuwa hapo awali,” alisema Bi. Mlimuka.

Mamlaka ya Elimu Tanzania kupitia mradi wake wa kukarabati  shule kongwe za Sekondari za Serikali unalenga kuimarisha Sekta ya Elimu nchini hasa kwa Shule za Serikali ambazo zilipoteza hadhi yake iliyokuwa hapo awali pamoja na kufadhili miradi mbalimbali ya elimu katika ngazi za Sekondari na Elimu ya Msingi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad