HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 14 July 2017

WAFANYAKAZI BOHARI KUU ZANZIBAR WAPATIWA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA JANGA LA MOTO

 Mkurugenzi Idara ya Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar Zahrani Ali Hamad akifungua mafunzo ya siku moja ya kukabiliana na janga la moto kwa wafanyakazi wa Idara hiyo Ofisini kwao Maruhubi Mjini Zanzibar.
  Kaimu Afisa wa mafunzo Kikosi cha Zimamoto Zanzibar Inspekta Ibrahim Ali Hassan akionyesha utaratibu bora wa kubeba chupa ya gesi kwa ajili ya kuzima moto katika mafunzo ya wafanyakazi wa Bohari Kuu ya dawa Maruhubi.
 Mmoja wa wafanyakazi wa bohari kuu ya dawa Zanzibar Ali Othman Omar (kushoto) akiuliza suala kuhusu matumizi sahihi ya mtungi wa kuzimia moto katika mafunzo hayo.
Fatma Omar Said akiwa katika mafunzo ya vitendo ya kukabiliana na janga la moto katika mafunzo ya wafanyakazi wa Bohari kuu ya dawa Zanzibar yaliyofanyika Maruhubi Mjini Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar
Sehemu zenye mikusanyiko ya watu zikiwemo Taasisi za Serikali na watu binafsi zinatakiwa kuwa na vifaa vya huduma ya kwanza vya kupambana na janga la moto na watu wenye taaluma ya kutumia vifaa hivyo.
Kaimu Afisa wa mafunzo Inspekta Ibrahim Ali Hassan wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar amesema sheria No. 7 ya mwaka 1999 ya Idara hiyo imewapa uwezo wa kuzifungia sehemu hizo iwapo zitashindwa kuweka vifaa na watu wenye uwezo wa kuzima moto.
Inspecta Ibrahim ametoa maelezo hayo alipokuwa akitoa mafunzo ya kukabiliana na moto kwa wafanyakazi wa Idara ya Bohari Kuu ya dawa Maruhubi.
Amesema lengo la kuwepo sheria hiyo ni kujaribu kuokoa maisha ya wananachi na mali zao wakati wa janga la moto ambalo linasababisha athari kubwa katika jamii.
Hata hivyo amesema bado taasisi nyingi za Serikali na binafsi hazijaona umuhimu wa kuweka vifaa vya huduma ya kwanza vya kuzimia moto na kuwapa mafunzo wafanyakazi wao .
Ameipongeza Wizara ya Afya kwa kujali kuwapatia mafunzo ya kukabiliana na moto wafanyakazi wa vitengo vyake mbali mbali na kuimarisha huduma hiyo katika taasisi zake kila mwaka.
Katika kukabiliana na janga la moto, Inspekta Ibrahim Ali Hassan aliwataka wafanyakazi wa bohari kuu kuacha fadhaa na kutumia njia za kitaalamu kwa kuondosha vitu ambavyo havijaanza kuungua, kuunyima moto hewa na kutia maji kwa moto wa kuni.
Aidha amewashauri wananchi kuanzisha utaratibu wa kuweka chupa ya kuzimia moto katika majumba yao na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar kinatoa mafunzo ya matumizi sahihi ya kifaa hicho bila malipo.
Amesema binadamu hawezi kuishi bila kutegemea moto na moto ni adui mpenzi wa binadamu hivyo tahadhari inahitajika wakati wote katika kujilinda.
Akizindua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Bohari Kuu ya dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad ametaka kila  mfanyakazi wa taasisi hiyo kuwa na uwezo wa kujilinda na moto yeye mwenyewe na mali iliyopo ndani.
Amesema bohari kuu ni taasisi muhimu katika ustawi wa maisha ya wananchi wa Zanzibar na imeweka mkazo kuhusu mafunzo hayo kwa wafanyakazi wote hivyo amewashauri kuyapokea kwa umuhimu wake.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad