HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 20, 2017

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AZINDUA MFUMO WA BIOMETRICS NA KAMERA ZA CCTV KATIKA HOSPITAL YA RUFAA MKOA WA DODOMA

Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde,akizungumza na wafanyakazi wa Hospital ya Mkoa wa Dodoma hii leo.

Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde,akizungumza na wafanyakazi wa Hospital ya Mkoa wa Dodoma hii leo,wakati wa uzinduzi mfumo wa Biometrics na kamera za CCTV katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.
Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde,akibonyeza kitufe wakati wa kuzindua matumizi ya mfumo wa Biometrics na kamera za CCTV katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
MBUNGE wa Dodoma mjini Anthony Mavunde ameendelea kutatua kero katika sekta ya Afya jimboni humo ambapo leo amezindua matumizi ya mfumo wa Biometrics na kamera za CCTV katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,kufuatia hali hiyo wagonjwa wengi waliokuwepo hospital hapo walionekana wenye furaha na kuunga mkono jitihada za mbunge wao katika kusaidia kuboresha huduma za Afya katika hospital hiyo.

Akizungumza katika uzinduzi wa matumizi ya vifaa hivyo, Mavunde amesema ufungaji wa mifumo hiyo ni miongoni mwa jitihada zake za kuhakikisha huduma za afya katika jimbo hilo zinatolewa ipasavyo.

Mavunde ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira na Vijana amesema mfumo huo umefungwa na Ofisi ya Mbunge wa Dodoma na amelazimika kufunga vifaa hivyo kutokana na malalamiko ya muda mrefu ya wagonjwa kuwa wamekuwa wakitolewa lugha chafu na wauguzi.

Amesema pamoja na kamera hizo, pia umefungwa mfumo wa Biometrics(uchukuaji alama za dole gumba) ili kudhibiti watumishi ambao wamekuwa wakiondoka kabla ya muda na kuchelewa kuingia kazini.

“Kamera hizi zinarekodi sauti na kuchukua video ili kuondokana na malalamiko yaliyotolewa na wananchi na itakuwa ni rahisi kumbaini mtu atakayelalamikiwa na mgonjwa,”amesema Mavunde

Mavunde amesema fedha alizotumia kununulia Kamera hizo na mfumo wa Biometrics amezipata kwa kujibana katika mshahara wake lengo likiwa ni kutekeleza ahadi yake aliyowaahidi wananchi wakati wa Kampeni kutatua kero za afya.

Aidha amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wananchi hasa ukizingatia kwasasa Dodoma kuna ongezeko la watu kutokana na serikali kuhamia mkoani humo.

“Baadaye pia tutaweka mfumo wa kuhifadhi mafaili, hii yote ni kurahisisha utendaji kazi katika hospitali hii ili wananchi wetu waweze kupata huduma za afya ipasavyo.pia nimeomba vifaa mbalimbali vya kisasa Ujerumani kwa ajili ya hospitali hii tukipatiwa itasaidia sana utoaji huduma za afya,”amesisitiza Mavunde

Amesema ameahidi kutatua changamoto katika sekta ya afya ambapo mbali na ufungaji vifaa hivyo alishakabidhi vitanda katika Zahanati na Vituo vya afya 35

“Nimetoa madawa kwenye kituo cha afya cha Makole yenye thamani ya Sh. Milioni 15,nimefunga umeme wa jua katika vituo vya Afya 17 pamoja na huduma za macho kwa watu 7000 na watu 3000 walipata huduma za upasuaji bure,”amesema

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Caroline Damiani amemshukuru Mbunge huyo huku akidai kuwa matunda ya ufungaji wa kamera yameanza kuonekana kwa watumishi kufanya kazi zao kwa ufanisi wa hali ya juu tofauti na awali.

“Kumekuwa na kero nyingi kutoka kwa wagonjwa sasa Kamera za CCTV zitatusaidia kutatua kero hizi na kudhibiti wale wanaotoka kabla ya muda wa kazi kuisha au kuchelewa kazini,”amesema Mganga huyo

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ya Entersoft Limited,Keneth Yindi amesema wamefunga Kamera 4 pamoja na mfumo wa Biometrics katika hospitali hiyo na ina uwezo wa kurekodi matukio kwa miezi tisa mfululizo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad