HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 10 May 2017

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR, BALOZI SEIF AWASILISHA HOTUBA YA MAKADIRIO NA MATUMIZI YA OFISI YAKE KATIKA KIKAO CHA BARAZA LA WAWAKILISHI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 katika Kikao cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar kilichoanza leo katika Majengo ya Baraza hilo yaliopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi ya Manaibu Mawaziri wa SMZ na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Baadhi ya Manaibu Mawaziri wa SMZ na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Timu ya Uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ukiongozwa na Katibu Mkuu wake Nd. Joseph Abdulla Meza wa Nne kutoka kulia wakiandika dondoo wakati wa Hotuba ya Ofisi yao ikiwasilishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu Mh. Simai Mohamed Said wa kwanza kutoka Kulia na Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake Mheshimiwa Suleiman Sarahan Said wakiwa makini kufuatilia Hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyowasilishwa Barazani. 
Picha na – OMPR – ZNZ.Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuimarisha zaidi huduma za Kijamii zikiwemo Elimu, Afya, Makaazi na upatikanaji wa Maji safi na salama katika azma yake ya kutoa kipaumbele kwenye mpango wake wa maendeleo katika kipindi cha mwaka 2017/2018.


Mpango huo utakwenda sambamba na uimarishaji wa Miundombinu ya uingiaji Nchini inayojumuisha Bandari, Viwanja vya Ndege , bara bara za ndani , Nishati pamoja na Tafiti zitakazosaidia kutoa maamuzi katika mipango hiyo ya Maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika Kikao cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar kilichoanza leo katika Majengo ya Baraza hilo yaliopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kugharamia uendeshaji wake na kutoa huduma bora kwa Wananchi kwa kutumia rasilmali zilizopo kwa umakini mkubwa na kuhakikisha matumizi yote yanaleta tija kwa Umma.

Alisema utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020 ikiwa katika kipindi cha mwisho cha miaka mitano unaenda sambamba na uidhinishwaji wa awamu ya Tatu ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini { MKUZA 111}.
Balozi Seif alieleza kwamba hiyo inamaanisha wazi kwamba Malengo ya Taifa bado yanadhamiria utekelezaji wa Mipango hiyo Mikuu ambayo imekusudia kukuza Uchumi, kuimarisha huduma za Jamii pamoja na kuimarisha Demokrasia na Utawala Bora.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba hali ya ukuaji wa uchumi wa Nchi imepelekea kuongezeka kwa Pato la Taifa kwa mwaka 2016 ambalo limeongezeka na kufikia thamani ya Shilingi 2,309.5 Bilioni ikilinganishwa na thamani ya shilingi 1,633.0 Bilioni Mwaka 2015.

Alisema uchumi wa Zanzibar umeimarika kwa asilimia 6.8 mwaka 2016 kutoka asilimia 6.5 mwaka 2015 hali iliyo tofauti na taswira inayojionyesha kwa mwenendo wa ukuaji wa Uchumi kwa Nchi za Kusini mwa Jangwa na Sahara ambapo kasi ya ukuaji wa uchumi imeshuka na kufikia wastani wa asilimia 1.6 mwaka 2016 kutoka wastani wa asilimia 3.4 mwaka 2015.

Akigusia mvua za masika zinazoendelea kunyesha hapa Nchini na kuleta athari kubwa kwa Wananchi walio wengi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwatahadharisha Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo miripuko ya maradhi yanayosababishwa na uchafuzi wa maji.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inawasisitiza Wananchi kuepuka kujenga katika maeneo hatarishi ambayo mazingira yake yanaweza kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa hasa wakati wa mvua kubwa zinazonyesha kama mabondeni, kwenye njia za asili za maji na pembezoni mwa milima hasa Kisiwani Pemba.

Balozi Seif alitoa wito kwa wananchi kuendelea kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya juu ya usafi wa mazingira ikiwemo kunawa mikono mara watokapo kujisaidia na kabla ya kula.

Kwa upande wa wafanyabiashara Balozi Seif aliwakumbusha kuendelea kufuata masharti yaliyowekwa juu ya biashara zao kwa kuzingatia suala la usafi na ulinzi wa afya za Wananchi ili kujikinga na maradhi ya mripuko.

Akigusia janga a dawa za kulevya linaloendelea kuiathiri jamii Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali yaMapinduzi ya Zanzibar kupitia Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya imetoa mafunzo kwa wadau katika shehia zenye Banadari Rasmi na zisizo Rasmi.

Alisema hatua hiyo ililenga kuweka wazi mbinu mbali mbali zinazotumiwa na wahalifu katika kupitishia dawa za kulevya ambapo washiriki wa mafunzo hayo wapatao 186 walitoa kwenye Shehia zipatazo 94 zenye Bandari hizo.

Balozi Seif alisema Kamati ya Kitaalamu ya Tume hiyo iliweza kupanga mikakati ya udhibiti wa dawa za kulevya, uimarishaji wa kinga dhidi ya matumizi ya dawa hizo pamoja na kuzisaidia Nyumba za upataji nafuu kwa vijana walioathirika na dawa za kulevya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza Nchi Rafiki, Taasisi, Makampuni na washirika wa maendeleo ndani na nje ya Nchi waliojitolea kuunga mkono harakati za Maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar na kupiga hatua kubwa Kiuchumi na ustawi wa Jamii.

Balozi Seif alisema michango ya washirika na Mataifa hayo marafiki imewezesha kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa huduma bora za Kijamii na kuleta maendeleo katika Taifa zima.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliliomba Baraza la Wawakilishi liidhinishe jumla ya shilingi Bilioni 44,837,577,000/- kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Taasisi zake kwa ajili ya kutekeleza Programu zake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

10/5/2017.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad