HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 13, 2017

Sehemu ya Kwanza -MAMBO USIYOYAFAHAMU KUHUSU NYERERE -

A: MAJINA YAKE

i. Kambarage

Kwa mila na tamaduni za kizanaki, Kambarage ni jina apewalo mtoto aliyezaliwa siku ya mvua. Mwalimu Julius Nyerere alizaliwa usiku wa mvua kali, Aprili 13, 1922 hivyo akaitwa Kambarage. Kambarage maana yake ni mzimu wa mvua.

ii. Julius

Aliendelea kulitumia jina la Kambarage mpaka 1942 alipobatizwa na kuwa mkristo rasmi. Alilichagua jina la Julius akivutiwa na mtawala wa zamani wa milki ya Roma, Julius Kaizari(Caesar) na ndipo akaitwa Julius Kambarage Nyerere kwa sababu hakutaka kuliacha kabisa jina lake la asili kwa kuwa tayari lilikuwemo kwenye rekodi zake za shule.

Alichelewa sana kubatizwa kwa sababu wamisionari walihisi angerithi uchifu wa baba yake. Kwa kawaida machifu huoa wanawake wengi kwa hivyo ubatizo wao usingekuwa na maana. Mwaka 1942, baba yake, Chifu Burito Nyerere alifariki, na uchifu ukarithiwa na kaka wa Kambarage aliyeitwa Edward Wanzagi. Wamisionari wakapata nafasi ya kumbatiza. Alibatizwa akiwa anasoma Tabora.

B: TANGANYIKA ONE

Alianza shule ya msingi 1934 akiwa na miaka 12. Alichelewa kuanza kwa sababu baba yake hakutaka mwanaye asome. Akiwa na miaka 11, alicheza bao na kumfunga mzee mmoja, rafiki wa baba yake. Huyo mzee akamshauri Chifu Burito kumpeleka mwanaye shule, mzee akakubali. Alianza mwezi Aprili wakati wenzake walianza tangu Januari. Alipoanza, alikuwa hajui hata Kiswahili lakini haikupita muda akajua.

Wakati huo, shule zilianzia darasa la kwanza mpaka la nne baada ya hapo kunakuwa na shule nyingine ya kuanzia darasa la tano mpaka la nane.  Kwa hiyo alitakiwa asome miaka minne halafu afanye mtihani wa taifa lakini kutokana na uwezo wake, alisoma miaka mitatu pekee kwani alipomaliza darasa la pili 1935, alirushwa mpaka la nne na kufanya mtihani wa taifa 1936 ambao aliongoza Tanganyika nzima.

C: MTETEZI WA HAKI

Mwaka 1937 alianza darasa la tano Tabora. Walimu wakampa cheo cha KAKA(kiranja). Kulikuwa na utaratibu wa makaka kupata upendeleo wa kujigawia chakula. Alipopewa cheo hicho, akaanzisha harakati za kuleta haki sawa kwa wote. Katika kutekeleza hilo, aliitisha mgomo kwa wanafunzi wote mpaka upendeleo ule uondolewe na akafanikiwa.

cc. Zaka Zakazi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad