HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 15 March 2017

VIONGOZI WAKUU NA WAJUMBE WA KAMATI KUU CHADEMA KUANZA ZIARA KATIKA MAJIMBO YA KANDA PWANI

Viongozi Wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wajumbe wa Kamati Kuu pamoja na wabunge, wataanza ziara ya kikazi itakayohusisha vikao vya ndani katika majimbo ya Kanda ya Pwani, ikiwa ni sehemu ya uimarishaji wa chama hicho na maandalizi ya uchaguzi wa kanda hiyo utakaofanyika Machi 19, mwaka huu.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chama hicho, Tumaini Makene imeeleza kuwa ziara hiyo ambayo itakuwa ni ya siku nne kwenye majimbo hayo itaanza Machi 16-17, itafuatiwa na Kikao cha Kamati Kuu Machi 18 na kufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi za Mwenyekiti wa Kanda, Makamu Mwenyekiti wa Kanda na Mweka Hazina wa Kanda, kisha Mkutano Mkuu Maalum wa Kanda ya Pwani inayohusisha mikoa ya Pwani, Temeke, Ilala na Kinondoni hapo Machi 19, kuchagua viongozi katika nafasi zilizotajwa.

Mbali ya agenda ya ukaguzi wa chama na uchaguzi wa kanda, vikao hivyo pia vitajadili hali ya kisiasa katika maeneo husika na taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe ataongoza timu itakayofika katika majimbo ya Kibaha Mjini na Segerea, Makamu Mwenyekiti wa Chama Tanzania Bara Prof. Abdalla Safari ataongoza timu katika majimbo ya Mkuranga na Temeke.

Makamu Mwenyekiti wa Chama (Zanzibar) Said Issa Mohamed ataongoza timu katika Jimbo la Ubungo huku Katibu Mkuu wa Chama Dkt. Vincent Mashinji akiongoza timu katika majimbo ya Kibaha Vijijini na Ukonga.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Tanzania Bara, John Mnyika ataongoza timu katika majimbo ya Bagamoyo na Mbagala huku Naibu Katibu Mkuu wa Chama Zanzibar akiongoza timu katika majimbo ya Mafia na Kawe.

Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye ataongoza timu katika majimbo ya Chalinze na Kinondoni, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa ataongoza timu katika majimbo ya Kisarawe na Kibamba.

Mjumbe wa Kamati Kuu Profesa Mwesiga Baregu ataongoza timu katika majimbo ya Kibiti na Kigamboni huku Mjumbe wa Kamati Kuu Halima Mdee akiongoza timu kwenye majimbo ya Rufiji na Ilala.

Wajumbe wengine wa Kamati Kuu watakaokuwa katika ziara hiyo ni pamoja na; Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Arcado Ntagazwa, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Hashim Juma Issa, John Heche, Joseph Mbilinyi, na Boniface Jacob.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad