HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 20 February 2017

SERIKALI WATOA TAMKO KWA BODI YA LIGI, YATAKA AMANI KATIKA MECHI YA JUMAMOSI

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Serikali imewataka bodi ya ligi kufanya maamuzi sahihi katika kuchagua  waamuzi wenye uwezo mkubwa wa kutafsiri sheria 17 za soka kwenye mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga utakaofanyika Jumamosi ijayo kwenye uwanja wa Taifa ili kuzuia athari ambazo zinaweza kujitokeza ikiwemo uharibifu wa mali za uwanja.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa michezo kutoka Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na michezo Yusuph Singo leo Jijini Dar es salaam ikiwa ni katika maandalizi ya kuelekea mechi ya watani wa jadi na kuwaasa viongozi wa bodi ya ligi kufanya maamuzi sahihi ili kuepusha vurugu zitakazoweza kujitokeza.

Singo alisema kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Oktoba mosi mwaka jana na kushuhudiwa vurugu kubwa zilizopelekea viti 1781 kuvunjwa, zilitokana na maamuzi mabovu ya waamuzi wa mchezo huo.

“Tunaitaka bodi ya ligi kupanga waamuzi wazuri kwenye mchezo huu kwakuwa unavuta hisia za watu wengi na pia tunawaomba mashabiki kuwahi mapema na kutojihusisha na vurugu zozote kwani ulinzi utakuwa wa kutosha” alisema Singo.

Kwa upande mkuu wa kitengo cha ulinzi na usalama wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Inspekta Hashim Abdallah alisema ulinzi utaimarishwa vya kutosha na wale wote watakaovunja sheria watachukuliwa hatua stahiki ukizingatia uwanja wa huo umefungwa kamera maalum kwa ajili ya ulinzi.

“Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kushangilia timu zao kwa amani lakini watakao jihusisha na vurugu tutawashughulikia ipasavyo” alisema Inspekta Hashim.

Wakati huo huo mtendaji mkuu wa bodi ya ligi, Boniface Wambura amevitaja viingilio hivyo kuwa viti vya bluu na kijani itakuwa shilingi 7,000 viti vya ‘orenji’ itakuwa shilingi 10,000, VIP B na C itakuwa shilingi 20,000 huku VIP A ikiwa ni shilingi 30,000.

Mbali na hilo, uongozi wa uwanja huo uliweza kuwapeleka waandishi katika chumba chenye mitambo ya kamera za ulinzi (CCTV) ambapo takribani uwanja mzima kuna kamera 119 zilizozunguka kila sehemu.
Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na michezo Yusuph Singo akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maandalizi ya mechi ya Simba na Yanga utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa. Kushoto ni Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura.
Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na Usalama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Inspekta Hashim Abdallah akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maandalizi ya mechi ya Simba na Yanga utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa na kutoa rai kwa mashabiki wa timu hizo kuja kwa ustaarabu.
Waandishi wa habari wakiwa wanapata maelekezo ya namna kamera zilizopo uwanjani zinavyotumika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad