HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 2 February 2017

CHANZO CHA KUZOROTA UTENDAJI BOMBA LA TAZAMA CHATAJWA

Imeelezwa kuwa kusuasua kwa utendaji wa Kituo cha Kusafisha Mafuta cha Indeni Petroleum Refinery Limited cha Ndola, nchini Zambia ni sababu mojawapo iliyochangia kuzorota kwa ufanisi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta la TAZAMA.

Hayo yemeelezwa hivi karibuni Jijini Dar es Salaam na Mawaziri wa Nishati wa Tanzania na Zambia mara baada ya kukamilisha ziara ya siku nne ya kutembelea mkuza wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la TAZAMA na Vituo vya Kusukuma Mafuta na kuzungumza na wafanyakazi wa vituo hivyo.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alibainisha kwamba kiwango cha Bomba kimeshuka ikilinganishwa na hapo hapo awali kwani lilikuwa na  uwezo wa kusafirisha lita za ujazo tani milioni 1.1 za mafuta kwa mwaka lakini kwa sasa linasafirisha lita za ujazo tani 600,000 tu.

Alisema usafishaji wa Mafuta unaofanywa na Kituo hicho cha Indeni hauendani na Usafirishaji wa Bomba la TAZAMA na hivyo kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia Bomba hilo kutofikia malengo.

Aliongeza kuwa, wakati mwingine inalazimu Pampu za kusukuma mafuta kuzimwa kwani mitambo ya kusafisha inakuwa haifanyi kazi na wakati huo huo matenki ya TAZAMA huko Ndola yanakuwa yamejaa na hivyo hakuna mahala pa kuhifadhi mafuta hayo.

Aidha, Waziri Muhongo alitaja sababu nyingine inayosababisha Bomba hilo kufanya kazi chini ya kiwango kuwa ni matumizi ya teknolojia ya kizamani ya tangu kujengwa kwake Mwaka 1968 ambayo haijabadilishwa katika maeneo mengi.

Alisema mradi huo wa TAZAMA una jumla ya Vituo Saba vya Kusukuma Mafuta (pumping stations), Vitano vikiwa upande wa Tanzania na Viwili vikiwa nchini Zambia lakini ni vituo viwili tu ndivyo ambavyo vimefungwa mitambo ya kisasa huku vingine vikiendelea kutumia teknolojia hiyo ya tangu Mwaka 1968.

“Katika vituo vyote vya TAZAMA, ni vituo viwili tu ndivyo vimebadilishwa pampu ambavyo ni Elphons Pass-Mikumi na Kigamboni huku vingine vyote bado vikiendelea kutumia teknolojia iliyopitwa na wakati,” alisema Waziri Muhongo.

Hata hivyo, alibainisha mipango na hatua mbalimbali zinazopaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha Bomba hilo linaboreshwa ambapo alisema kuwa, hivi sasa kwa upande wa Serikali ya Zambia ni kuboresha Bomba la Mafuta sambamba na Kituo hicho cha Indeni ili kuwe na uwiano na hivyo kufikia malengo kwa pande zote mbili.

“TAZAMA haitakufa; inapaswa kufanya kazi kibiashara ambapo kunahitajika mtaji, teknolojia na ubunifu ili iweze kushindana,” alisema Profesa Muhongo.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David aliongeza kwamba, uboreshaji huo unahitaji kwenda sambamba na mabadiliko ya kimtazamo ya wafanyakazi wa TAZAMA.

Alisema, hata kama teknolojia itabadilishwa ni lazima wafanyakazi nao wabadilishe utendaji wao wa kazi na hivyo kuwataka kuacha mara moja kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuwa wabunifu na wajitume ili kuleta matokeo chanya.

“Tumeona mnao uwezo wa kubadilika; kwa maana tumeshuhudia namna mnavyojitahidi kutunza miundombinu ambayo ilifungwa zamani wakati Bomba linaanza kazi lakini hadi leo bado vinafanya kazi,” alisema Waziri David.

Waziri David aliwahakikishia wafanyakazi hao kwamba Serikali zote mbili zitaendelea kutoa ushirikiano kila inapobidi na kuwa zimedhamiria kwa dhati kuhakikisha TAZAMA inabadilika na kuwa ya kisasa zaidi.

Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David akizungumza na Wafanyakazi wa TAZAMA, Kituo cha Kigamboni. Katikati ni Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TAZAMA, Davison Thawethe (kushoto) akizungumza wakati wa ziara ya Mawaziri wa Nishati wa Uganda na Tanzania ya kutembelea Bomba na Vituo vya Kusukuma Mafuta Ghafi vya kampuni hiyo. Kulia ni Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David na Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo (katikati).
Baadhi ya Wafanyakazi wa TAZAMA- Kituo cha Kigamboni wakiwasikiliza Mawaziri wa Nishati wa Tanzania na Zambia (hawapo pichani) walipofanya ziara kituoni hapo na kuzungumza nao.
Pumpu mpya ya Kusukuma Mafuta Ghafi ya Kituo cha Elphons Pass-Mikumi. Katika vituo vyote vya Kusukuma Mafuta vya TAZAMA, ni vituo viwili tu ndivyo vimebadilishwa pampu ambavyo ni Kigamboni na Elphons Pass.
Pumpu za Kusukuma Mafuta Ghafi za kituo kimojawapo cha Kampuni ya TAZAMA. Pampu hizo zilifungwa tangu Mwaka 1968.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa akizungumza na Wafanyakazi wa Kituo cha TAZAMA- Kigamboni. Katikati ni Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad