HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 23, 2017

AZAM VS COSMOPOLITAN LEO, BOCCO KUIPA HESHIMA TIMU YAKE YA ZAMANI


Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii


KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo saa 10.00 jioni itakuwa kibaruani kupambana na Cosmopolitan katika mchezo wa raundi ya tano ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.


Azam FC inaingia kwenye mchezo huo  leo ikiwa imejidhatiti vilivyo kuweza kuanza vema kwa kupata ushindi na kuitupa nje timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (SDL) na kutinga raundi ya 16 bora. Kwa muda wa siku tatu, Azam FC imefanya mazoezi makali kujiandaa na mchezo huo, na itakumbukwa kwenye mtanange wa mwisho iliyotoka kucheza ukiwa ni wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), matajiri hao walilazimishwa suluhu ya bila kufungana na Mbeya City.

Kuelekea mchezo huo Nahodha wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’, atakuwa akirejea kucheza dhidi ya timu yake hiyo ya zamani ambayo ndiyo imemtoa hadi kupata nafasi ya kusajiliwa na Azam FC miaka tisa iliyopita wakati ikishiriki ligi ya madaraja ya chini na kuipandisha rasmi Ligi Kuu mwaka 2008 baada ya kufunga mabao mawili yaliyoipandisha daraja Azam FC walipoichapa Majimaji ya Songea 2-0.

Nahodha huyo Msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, amepanga kuipa heshima maalumu Cosmopolitan leo kwa kutoshangilia bao atakalofunga kutokana na kutambua mchango wao wa kumtoa hadi kusajiliwa na Azam FC.

“Ni jambo zuri sana kucheza dhidi ya timu yako ya zamani, najisikia furaha sana ni moja ya mchezo mzuri kwangu na nitacheza kwa nguvu ili niweze kuisaidia timu yangu iweze kupata matokeo mazuri, siwezi kushangilia nikifunga bao, ile ni timu yangu ambayo imenitoa,” alisema.

Bocco alisema kuwa wao kama wachezaji wanamorali kubwa kwa ajili ya kucheza mchezo huo, huku akidai kuwa wamejipanga kupambana uwanjani kuhakikisha wanashinda mtanange huo. “Maandalizi mazuri, tumemaliza mazoezi ya mwisho, kwanza mchezo utakuwa mgumu timu tunayocheza nayo ni timu ya madaraja ya chini, lakini naamini itakuwa imejiandaa vema, sisi tutaenda kupambana ili kuibuka na ushindi, ukizingatia lazima tushinde mchezo huo ili tuweze kusonga kwa raundi inayofuatia,”..

Hii ni michuano ya pili ya FA Cup kwa Azam FC kuweza kushiriki tokea ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008/2009, ya kwanza ilikuwa msimu uliopita ambapo ilifanikiwa kufika hadi fainali, lakini haikuwa na bahati ya kubeba taji hilo baada ya kufungwa na Yanga mabao 3-1.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad