Maafisa wa serikali za Kenya na Tanzania, waliokutana mjini Naivasha, nchini Kenya, Januari 18 – 22 mwaka huu, wameazimia kutekeleza uimarishaji wa mpaka wa nchi hizo, unaokadiriwa kufikia kilometa 760, kwa awamu.
Kiongozi wa ujumbe wa serikali ya Tanzania kwenye mazungumzo hayo, Bw. Justo Lyamuya, amesema zoezi hilo linatarajiwa kuanza Aprili mwaka kuu na kipande cha Ziwa Victoria mpaka Ziwa Natron (kilometa 238).
Akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. John Haule, jijini Nairobi mwishoni mwa juma, Bw. Lyamuya, ambaye ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, alisema utekelezaji wa mradi huo utategemea upatikanaji wa fedha zinazokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 4.68 (Shilingi bilioni 5.13), gharama ambayo itagawanwa na serikali za Kenya na Tanzania.
Mpaka wa Kenya na Tanzania unaanzia pembezoni mwa Ziwa Victoria na kuishia Bahari ya Hindi eneo la Vanga.
No comments:
Post a Comment