HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 23, 2013

NYATI ALIYEJERUHI WILAYANI MAKETE ASAKWA


Na Edwin Mushi 
wa Globu ya Jamii, Makete
Jitihada za kumuua nyati aliyemjeruhi mkazi mmoja wa kijiji cha Ilevelo wilayani Makete kwa takribani siku tatu mfululizo linaonekana kugonga mwamba baada ya mnyama huyo kutafutwa bila mafanikio.

Zoezi hilo linaloendeshwa chini ya Idara ya maliasili ya halmashauri ya wilaya ya Makete kwa kushirikiana na askari wanyama pori, limeonesha kutokuzaa matunda kutokana na kumtafuta mnyama huyo bila mafanikio hali inayosababisha kutishia usalama wa wakazi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani.

Akizungumza na mwandishi wetu aliyepo eneo la tukio, Bw. Lulesu kutoka idara ya maliasili wilaya ya Makete amesema juzi walifanikiwa kumuona mnyama huyo na wakati wakifanya jitihada za kumuua aliwatoroka na kumtafuta bila mafanikio hali iliyopelekea zoezi hilo kuahirishwa hadi jana alhamisi ambapo pia walimtafuta bila mafanikio.

Amesema kwa hivi sasa baada ya leo hii kumtafuta bila mafanikio wanadhani huwenda mnyama huyo amehamia vijiji vya jirani ikiwemo Imehe na Luwumbu na kutoa rai kwa wakazi wa vijiji hivyo kuchukua tahadhari hasa wakati wa kwenda kwenye shughuli za kilimo

Kutokana na hali hiyo ya sintofahamu kuwagubikwa mashaka makubwa kumepelekea wananchi hao kuishi maisha ya wasiwasi na kuishukuru halmashauri ya wilaya ya Makete na wote waliofika kwa ajili ya zoezi la kumuua nyati huyo, kwani kitendo hicho kimeonesha kuwa serikali yao inawajali.

Miongoni mwa viongozi waliopongezwa kwa kushinda na wananchi hao kwa siku ya jana ni mkurugenzi mtendaji wa hallmashauri ya wilaya ya Makete Iddi Nganya, ambaye alishinda nao kumtafuta nyati huyo bila mafanikio.

Uongozi wa timu inayoendesha zoezi hilo umetoa rai kwa wananchi wa Ilevelo na vijiji vya jirani ikiwemo Imehe na Luwumbu kutembea kwa makundi na kuchukua tahadhari kubwa kipindi hiki ambapo nyati huyo ametoweka katika mazingira ya kutatanisha na kudhaniwa huwenda ameelekea kwenye vijiji jirani.

Wiki iliyopita mkazi wa kijiji cha Ilevelo kata ya Lupalilo wilayani Makete Bw Alfred Sanga alijeruhiwa na mnyama huyo, na kupatiwa matibabu katika hospitali ya Ikonda Consolatha ambapo hivi sasa afya yake inaendelea vizuri

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad