HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 28, 2013

POLISI MAKETE LAWAMANI

Na Edwin Moshi, Makete

Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani wilayani Makete mkoani Njombe limeingia lawamani kufuatia kutwishwa tuhuma nzito za kutoza faini kwa madereva pikipiki bila kuwapa risiti ya fedha hizo.

Baadhi ya madereva bodaboda waliozungumza na mtandao huu wamesema wamekuwa wakikamatwa na askari hao wa usalama barabarani huku akimtaja kwa jina askari ambaye amekuwa kinara wa kuwatoza faini bila kuwapa risiti (jina tunalihifadhi kwa sasa).

Tuhuma hizi zimetolewa kwenye mkutano wa hadhara wa CCM kwenye kijiji cha Ndapo na Kinyika wilaya ya Makete ulioongozwa na mwenyekiti wake Bw. Francis Chaula uliofanyika katika kata ya Matamba wilayani hapo ambapo pamoja na mambo mengine aliruhusu wananchi kutoa kero zao ndipo lilipoibuka suala hilo.

Wamesema wamekuwa wakitozwa faini ya zaidi ya shilingi laki tatu pasipo kupewa risiti na pindi wanapohoji huambulia kipigo kutoka kwa askari hao.

Akizungumza wakati wa kujibu suala hilo mwenyekiti wa CCm wilayani hapo Bw Francis Chaula amesema askari hao hawana haki ya kuwapiga madereva hao na pia kitendo wanachokifanya cha kutoza faini bila risiti ni kinyume na utaratibu wa serikali hivyo kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja.

Amesema kufuatia tuhuma hizo viongozi wa jeshi la polisi wilayani hapo wanatakiwa kuchukua hatua haraka na endapo askari hao watabainika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Jeshi la polisi kupitia kwa afisa upelelezi wake Bw. Gosbert Komba akizungumza kwa niaba ya mkuu wa polisi wilaya amesema vitendo hivyo havikubaliki kisheria huku akiongeza endapo suala hilo likichunguzwa na kubainika lina ukweli sheria itachukua mkondo wake kwa askari hao.

Bw Komba amesema madereva nao wana wajibu wa kuelewa sheria inasema nini hasa pale wanapokamatwa na makosa na kusema kuwa faini hulipwa kwenye kituo cha polisi na risiti ya malipo hayo hutolewa na kutaka kushirikiana na jeshi hilo kufichua wale wanaokiuka utaratibu huo ili wachukuliwe hatua.

Amesema kwa kufanya hivyo kutaepusha usumbufu usio wa lazima ikiwemo lawama zisizo za msingi ambazo zinaelekezwa kwa jeshi hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad