Wachezaji wa Klabu ya Kayumba wakishangilia na kitita cha Shilingi laki saba mara baada ya kukabidhiwa kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Taifa ya Safari Pool Mkoa wa kimichezo wa Ilala ngazi ya mkoa uliomalizika katika klabu ya Mashujaa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya mchezo wa pool ya Kayumba yenye makazi yake Buguruni katika Mkoa wa kimichezo wa Ilala, ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya pool ya 'Safari Lager National Pool Championship 2012' baada ya kuibamiza Mashujaa ya Vingunguti 13-8 katika mchezo wa fainali wa mashindano hayo ngazi ya mkoa yaliyofanyika katika Klabu ya Mashujaa Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Kayumba ilitwaa ubingwa huo na kujinyakulia fedha taslimu Sh.700,000 na pia kuwa wawakilishi wa mkoa huo katika fainali za Kitaifa zitakazofanyika Septemba mkoani Mwanza kwa kushirikisha vilabu 16 ambavyo vitakuwa mabingwa kwenye mikoa yao.
Mashujaa ilikamata nafasi ya pili na kuzawa kitita cha shilingi 350,000 na mshindi wa tatu katika mashindano hayo walikuwa ni Klabu ya La Familia ya Tabata Kimanga ambao walizawadiwa shilingi 200,000 na wanne ni klabu ya Titanic ya Vingungiti ambao walizawadiwa shilingi 100,000.
Upande wa mchezaji mmoja mmoja “Singles” (wanaume), Felix Athanas (Yeboyebo) kutoka klabu ya Mashujaa alitwaa ubingwa kwa kumchapa Goodluck Steven(Tetenus) wa klabu ya MC ya Tabata 5-3, na kujinyakulia kitita cha shilingi 350,000 ambapo Goodluck Steven alikamata nafasi ya pili na kuzawadiwa shilingi 200,000, wakati Samson Kibugsa wa klabu ya Mashujaa alikamata nafasi ya tatu na kuzawadiwa shilingi 150,000.
Upande wa mchezaji mmoja mmoja “Singles” (wanawake),Elizabeth Besti kutoka Klabu ya Sun Set ya Tabata Kimanga alitwaa Ubingwa na kuzawadiwa Shilingi 250,000/= kwa kumfunga Grace Gabna ambaye alikamata nafasi ya pili na kuzawadiwa shilingi 150,000/= na mshindi wa tatu alikuwa ni Rosemary Mathew wa klabu ya Mc ya Chan’ombe ambaye alijinyakulia shilingi 100,000.
Zawadi kwa washindi wote zilikabidhiwa na Mkurugenzi wa Diwani wa Kata ya Vingunguti,AssaaSimba ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha mashindano hayo katika Mkoa wa kimichezo wa Ilala
No comments:
Post a Comment