HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 13, 2012

Rais RT aifagilia Tabora Marathon

Rais wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Francis John (kati) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya utambulisho wa mbio za Tabora Marathon uliofanyika katika hoteli ya Lamada Apartments jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mratibu wa mbio hizo, Ramadhani Makula na Mshauri wa mbio hizo, Tullo Chambo.

Na Francis Dande

CHAMA cha Riadha Tanzania (RT), kimewapongeza waratibu wa Kamati ya maandalizi ya mbio za Tabora Marathon kwa kubuni na kuandaa mbio za kwanza kufanyika katika historia ya Mkoa wa Tabora.

Akizungumza katika hafla ya utambulisho rasmi wa mbio hizo iliyofanyika katika hoteli ya Lamada Apartments jijini Dar es Salaam, Rais wa RT, Francis John, alisema, Mkoa wa Tabora ni chimbuko la mchezo wa riadha hapa nchini, ingawaje hivi sasa ile chachu imepotea, hivyo kitendo cha waratibu hao kubuni na kuandaa mbio hizo ni cha kupongezwa na kuungwa mkono kwani kitaleta chachu mpya.

John alisema, RT kwa kutambua mchango wa Mkoa wa Tabora katika riadha, ndio maana RT iliamua kuadhimisha miaka 100 ya riadha duniani kitaifa mkoani humo, jambo lililochochea hamasa ya mchezo huo mkoani Tabora.

Alisema, kitendo cha waratibu hao kubuni na kuanzisha mbio hizo kinapaswa kuungwa mkono na wale wote wapenda michezo na kuigwa na mikoa mingine kwa manufaa ya riadha Tanzania.

“Sisi kama cha kitaifa kazi yetu si kubuni mashindano katika mikoa, hilo ni jukumu la wadau kwa kushirikiana na mikoa, hivyo kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Mkoa wa Tabora tunaunga mkono juhudi za waratibu hawa na tunatoa wito mikoa mingine kuiga mfano,” alisema na kuongeza.

Tabora ni chimbukoa la wanariadha wengi hapa nchini, zamani shule kama Tabora Boys na nyinginezo zilikuwa zikitoa wanariadha mahiri, lakini hivi sasa hali hii haiko tena, hivyo kwa matukio kama ya mbio hizi yatachochea kuurudisha Mkoa wa Tabora katika enzi zake.

Alitoa wito kwa wakazi wa Tabora, kuipokea vema na kuiunga mkono mbio hiyo kwani tukio muhimu kijamii ndani ya Mkoa huo.

Naye Mratibu wa Tabora Marathon, Ramadhani Makula, alisema, kutokana na kuwa mzaliwa wa Tabora kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Mkoa huo na maeneo ya jirani ndiko kumewasukuma kuandaa mbio hizo zenye lengo la kuibua vipaji na kutangaza vivutio vya kihistoria ya mkoa huo ikiwamo Livingstone Museum iliyoko Kwihala mjini humo, ambavyo kimsingi vimesahaulika na havipewi kipaumbele.

Makula alisema, katika mbio hizo zitakazofanyika Machi mwaka huu, pia washiriki watafanya shughuli za utunzaji mazingira ikiwamo upandaji miti katika makimbisho hayo ya Dk. Livingstone.

Mbio za Tabora Marathon zitashirikisha mbio za Nusu Marathon Kilomita 21 na zile za kujifurahisha za Kilomita 5, ambako hadi sasa wadhamini mbalimbali wameanza kujitokeza kuunga mkono tukio hilo ikiweko Kampuni ya Auric Air, NGS ya mkoani Shinyanga na Dash Communication ya Sinza jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad