HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 26, 2011

SHIRIKA LA UNDER THE SAME SUN LAIBANA TANZANIA KUHUSU MAUAJI YA ALBINO

Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Under The Same Sun (UTSS), hapa nchini, Vicky Ntetema akisalimiana na mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Majaliwa Ng'oyelwa, baada ya kukutana na mtoto huyo njiani katika mji wa Kasamwa Wilayani Geita mkoani Mwanza, jana. Kushoto kwake aliyesimama mbele ni Rais wa UTSS, Peter Ash na Paul Ash. Viongozi wa shirika hilo linalipiga vita mauaji ya albino walizuru wilayani Geita kwa ziara ya kikazi.

Na Mwandishi Wetu,Mwanza
SHIRIKA la Kimataifa la kutetea haki za watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), la Under The Same Sun (UTSS), limeitaka Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri wake Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kuutangazia ulimwengu kuhusu matokeo ya ripoti ya kura za maoni, dhidi ya watu wanaosadikiwa kuendesha mauaji ya walemavu hao.

Mbali na hayo, Shirika hilo lenye makao makuu yake nchini Canada, limeeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Serikali nchini kuwaruhusu waganga wa kienyeji kuendelea na kazi zao hizo, licha ya kudaiwa kuwa chanzo kikuu cha chimbuko la mauaji hayo ya kinyama.

Mkurugenzi wa Under The Same Sun hapa nchini, Vicky Ntetema, aliyasema hayo jana jijini Mwanza, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, wakati wa kongamano la kupiga vita mauaji ya albino nchini, lililofanyika Chuo cha SAUT, na kuwashirikisha wanafunzi wa Chuo hicho. 

Ntetema ambaye amejiwekea historia nzuri ya kubaini na kufichua chanzo cha mauaji ya albino hapa nchini, alisema Serikali ya Tanzania lazima iwatangazie wananchi wake ripoti ya kura hizo za maoni, ambazo ziliendeshwa kwa dhumuni la kuwafichua wahalifu hao.

"Shirika la Under The Same Sun, tunahoji kwa nini Serikali ya Tanzania imekumbatia na haitaki kutangaza ripoti ya kura za maoni juu ya watuhumiwa wa mauaji ya albino?. Na ni kwa nini iliruhusu waganga kuendelea na kazi zao, ulipokaribia Uuchaguzi Mkuu 2010?.

"Kama kweli Serikali ilidhamiria kuwasaka na kuwakamata watuhumiwa wa mauaji ya albino mbona imepatwa kigugumizi kutangaza waliotajwa?. Kuna nini hapa?. Tunataka ripoti hiyo itangazwe", alisema Ntetema ambaye amejizolea umaarufu kuhusiana na uchunguzi wake alioufanya mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhusiana na chanzo cha mauaji ya albino nchini. 

Mauaji ya maalbino nchini Tanzania bado yanaendelea, licha ya kuanzishwa kwa kampeni za kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaotumia viungo vya binadamu kwa imani za kishirikina. Taarifa zinasema kwamba, hadi sasa zaidi ya maalbino 20 wameuawa tangu mwishoni mwa mwaka jana, licha ya amri ya Rais Jakaya Kikwete kutaka walemavu hao wa ngozi walindwe, na watuhumiwa wawajibishwe kisheria. 

Ntetema ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, na amewahi kuwa mwakilishi wa Shirika la Utangazaji nchini Uingereza (BBC), hapa nchini, alihoji sababu za Serikali kuanza maandalizi mengine ya kuunda kikosi kazi za kufuatilia watuhumiwa wa mauaji ya albino, wakati ripoti ya kura za maoni ya awali imeshindwa kuyatoa kwa Umma.

Hata hivyo, Ntetema alilishukia Jeshi la Polisi lililopo chini ya Mkuu wake (IGP), Said Ali Mwema kwa madai kwamba limekuwa likiwalinda baadhi ya watuhumiwa wa mauaji ya walemavu hao wa ngozi. 

Akifafanua kuhusu hilo, alisema: "Kuna kesi moja huko mkoani Shinyanga polisi walipoteza ushahidi wa mtuhumiwa wa mauaji ya albino. Tunahisi kuna rushwa hapa, na pengine wanaohusika ni vigogo fulani ama matajiri, maana mtu masikini hawezi kufanya hivyo".

Kwa upande wake, Rais wa Shirika hilo la Under The Same Sun, Peter Ash, aliueleza ulimwengu kwamba, juhudi za maksudi bado zinahitajika kwa kila nchi katika suala zima la kuwalinda na kuwathamini albino, kwani watu hao ni binadamu kama walivyo wengine. "Mungu alimuumba albino si kwa makosa, bali alimuumba kwa mapenzi yake. 

Hivyo tunataka dunia itambue kwamba albino ni binadamu na anastahili kuheshimiwa, kuthaminiwa na kupewa haki zake zote za kibinadamu", alisema Rais Ash.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad