Rais Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akijadiana jambo na Mfalme MswatiIII wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa SADC unaofanyika SANTON, Johannesburg, Afrika ya Kusini.Katikati aliyesimama ni Mkuu wa Itifaki Balozi Antony Itatiro.Picha na Freddy Maro
Na Mwandishi Wetu.
Nchi Wanachama wa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) hivi karibuni wataanza kunufaika na fursa za kibiashara zitokanazo na kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara.
Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi Wanachama za Utatu wa COMESA-EAC–SADC unaotarajiwa kufanyika kesho (tarehe 12 Juni, 2011) katika ukumbi wa Sandton Convention Centre, Johannesburg, Afrika Kusini, utazindua rasmi majadiliano ya Eneo Huru la Biashara la Utatu wa Jumuiya hizo.
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za Utatu, unatarajiwa kupitia taarifa ya Mkutano wa Pili wa Baraza la Mawaziri wa Utatu wa COMESA – EAC – SADC, Kusaini Azimio na Kuzindua Rasmi Majadiliano ya Eneo Huru la Biashara la Utatu.
Ujumbe wa Tanzania unaoongozwa na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeshiriki katika mikutano yote ya maandalizi kabla ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi. Ujumbe umeshirikisha pia Mawaziri na Makatibu Wakuu kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar wakiwemo Mh. Dkt. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar, Mhe. Dkt. Abdulla Saadalla, Naibu Waziri Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Cyril Chami Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Nassor Ahmed Mazrui Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko Zanzibar.
“Nchi Wanachama wa Utatu wa COMSA-EAC-SADC zitaharakisha mchakato unaoendelea ili kufikia lengo lililokusudiwa la kuanzisha Eneo Huru la Biashara mapema iwezekanavyo, na kukuza utekelezaji wa mpango wa uendelezaji wa miundombinu na biashara” Alisisitiza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya kuwasili Mjini Johannesburg.
Utatu wa Jumuiya za COMESA-EAC-SADC unajumuisha Nchi Wanachama 23 ambazo ni zaidi ya nusu ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika. Eneo huru la biashara katika Utatu wa Jumuiya hizi lina idadi ya watu takriban millioni mia sita (Mil. 6), hii ikiwa ni fursa kubwa katika soko lililopanuka.
Nchi 19 Wanachama wa COMESA ni Burundi, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Djibouti, Egypt, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Libya, Madagascar, Malawi, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Sudan, Swaziland, Uganda, Zambia, Zimbabwe. Nchi 5 Wanachama wa EAC ni Burundi, Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Muungano waTanzania na Uganda.
Nchi 15 Wanachama wa SADC ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo (DRC), Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, Seychelles, South Africa, Swaziland, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

No comments:
Post a Comment