HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 4, 2010

WANAWAKE WATAKIWA KUJITOKEZA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI KATIKA UCHAGUZI MKUU UJAO!


Na Asteria Muhozya, Tabora

Naibu Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Juma Ali Shamhuna (pichani) amewata wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa Ujao.

Mhe. Shamhuna ambaye amemwakilisha Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Aman Abeid Karume, ameyasema hayo wakati akizindua Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani katika Uwanja wa Chipukizi Mkoani Tabora.

Aidha, ameeleza kuwa, ujio wa Azimio la Ulingo wa Beijing umeleta mabadiliko makubwa katika kuwapa wanawake fursa mbalimbali za uongozi na katika maeneo mengine ambayo yalianishwa wakati wa Mkutano wa Beijing, uliofanyika nchini China mwaka 1995. Na hivyo, Kuitaka jamii kuwaendeleza, na kuwaelimisha wanawake badala ya kuwaacha kuwa wafanyakazi wa shughuli za jikoni.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutoa nafasi za upendeleo kwa wanawake katika Uchaguzi Mkuu ujao ili kufikia asilimia 40% pamoja na ukweli kwamba, wanawake wengi wameonesha mwamko na mwitikio wa kujitokeza kugombea badala ya kusubiri nafasi hizo za upendeleo. Aidha, ameeleza kuwa, lengo la Serikali ni kufikia asilimia 50% ya uwakilishi wa wanawake katika ngazi za siasa na maamuzi.

Akitoa mfano wa Serkali ya Mapinduzi Zanzibar amesema, mara baada ya Mkutano huo wa Beijing, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweza kuongeza nafasi za uwakilishi wa wanawake kufikia asilimia 30%.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Mhe. Margaret Sitta wakati akitoa maelezo kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani amesema kuwa, maadhimisho ya mwaka huu yana madhumuni ya kupima utekelezaji wa Sera na program nyingine za Kitaifa na jinsi zinavyowiana na utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele yaliyotokana na Mkutano wa Ulingo wa Beijing ili kuweza kubaini mafanikio, changamoto na namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

Aidha, ameeleza kuwa, dhumuni lingine ni kuainisha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano cha uongozi wa awamu ya nne katika kutekeleza masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wanawake na Jinsia na kuongeza kuwa, maadhimisho haya yatatumika kuwahamasisha wanawake wenye sifa za uongozi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Halikadhalika Waziri Sitta ameongeza kuwa, maeneo hayo ya ulingo wa Beijing yamekuwa yakitekelezwa na Serikali kwa kupitia njia mbalimbali kama vile Mkakati wa Kukuza na Kuondoa Umaskini (MKUKUTA) pamoja na Sera mbalimbali. Aidha, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 inatamka wazi kuhusu utekelezaji wa haki za wanawake.

Akielezea zaidi kuhusu namna maadhimisho hayo yatakavyoadhimishwa Kimatafa amesema kuwa, maadhimisho hayo yatafanyika pia New York Marekani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon atatoa salam za maadhimisho hayo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, vilevile salam zake zitatolewa kupitia Wawakiishi wa Umoja wa Mataifa kwa kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, 2010 ni ‘’Miaka 15 baada ya Beijing: Wanawake Wanaweza Wapewe Nafasi’’.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad