HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 31, 2010

Mcheza Filamu Wa Siku Nyingi, Elizabeth Taylor Asema Amechoka Kufanyiwa Operesheni


Nimebahatika kuzaliwa na kuishi katika familia ya watu wakereketwa wa tasnia ya filamu. Niliona filamu ya kwanza nikiwa na umri wa miaka mitatu, na haikuwa kwenye Luninga kama tunavyozifahamu leo, ilikuwa ni kwenye jumba la senema pale mkoani Iringa. Hii ilikuwa ni miaka ya 80, na filamu ambayo ilikuwa na jina kubwa sana wakati huo ilikuwa ni "Disco Dancer" ya mzee mzima Tarvota.

Bahati hii ya kuzaliwa kwangu katika familia ya watu waliokuwa wakipenda kwenda kutazama na kufuatilia habari za filamu iliniwezesha kuanza kusikia majina makubwa ya waigizaji wa tasnia hii na moja ya jina lilokuwa likitamkwa sana kwenye maongezi lilikuwa ni Elizabeth Taylor.

Taylor alizaliwa nchini Uingereza na alianza shughuli zake za uigizaji kama muigizaji wa jukwaani (Theatre Actress) lakini umaarufu wake aliupata huko Hollywood, Marekani alikohamia kufanya kazi kama muigizaji wa filamu. Filamu zilizompatia umaarufu mkubwa ni pamoja na "Cleopatra", "Cat on a hot tin Roof", "National Velvet" na "Who's afraid of Virginia Woolf".

Umaarufu wake ulitokana na ulimbwende aliokuwa nao, pamoja na kicheko chake kilichokuwa kikipendwa na wanaume wengi, wapenzi wa filamu, ambao walisema kicheko cha muigizaji huyu kwa kiasi kikubwa kilikuwa kikiamsha hisia zao za kimapenzi.

Elizabeth Taylor, 78, hakupata umaarufu wake kwa kununua au kwa kuuza utu wake, mwanamama huyu aliujenga umaarufu wake kwa kufanya kazi usiku na mchana. Moja ya mafanikio yake makubwa ni kushinda tuzo mbili kubwa kabisa za tasnia ya uigizaji filamu duniani, tuzo za Oscar.



moja ya filamu alizocheza Mwana mama Elizabeth Taylor

Pamoja na mafanikio hayo makubwa na utajiri mkubwa alioupata kutokana na uigizaji filamu maisha yake halisi hayakukosa misukosuko, mingine ikiwa mikubwa kupindukia. Moja ya misukosuko hiyo ni kuolewa na kuachika mara nane. Lakini cha kushangaza ni kwamba kila alipoanguka Taylor hakukubali kubaki chini, aliinuka tena na kuendeleza libeneke kwa spidi kubwa kuliko ile ya awali.

Taylor kwa kipindi kirefu amekuwa akipambana na matatizo ya kiafya ambayo yamesababisha kufanyiwa operesheni zisizopungua 100 ndani ya miaka 25 pekee. Kwa sasa anasumbuliwa na matatizo ya uti wa mgongo ambao umemfanya asiweze kutembea kwa miguu yake mwenyewe na wakati mwingine kushindwa hata kuinua kichwa chake kwa maumivu.

Msaidizi wake wa karibu amesema, "Kwa sasa Eliza anatumia kiti cha magurudumu, na kuna wakati huegemeza kichwa chake kwenye bega lake siku nzima ili kupata nafuu ya maumivu yatokanayo na uti wa mgongo."

Pamoja na maumivu makali ambayo amekuwa nayo, Eliza amesema kwamba hayuko tayari kufanya oparesheni nyingine, amechoka na sasa anamwachia Muumba wake. Matatizo mengine ya kiafya ambayo Taylor amekuwa akipambana nayo ni uvimbe kwenye ubongo (Brain Tumor), Kisukari, Nimonia, Kansa ya Ngozi, Kifafa, na Stroke.

Taylor ameshafanyiwa upasuaji wa mapaja yake yote mawili, ameshapasuliwa mara tano kwenye uti wake wa mgongo, na pia amezaa mara tatu kwa kufanyiwa upasuaji mwaka 1954, 1955, na 1957. Mwaka jana alifanyiwa upasuaji wa moyo.

Ninachotaka kusema katika habari hii ni kwamba, kama wewe msomaji ulikuwa unadhani unaumwa sana basi jiulize tena kama unadhani unaumwa sana? Na pia ni lazima tufahamu kila kitu kina gharama yake, umaarufu na utajiri vikiwemo. Pengine mama huyu asingekuwa maarufu na tajiri anagekuwa ameshajipumzikia lakini kwa sababu kuna watu wanapata utajiri mkubwa kutokana na umaarufu na utajiri wake hawataki afe, wangependa aendelee kuwapo ili wafaidike zaidi.

Hongera Elizabeth Taylor kwa uamuzi wako mzuri wa kuamua kusimamia nafsi yako mwenyewe.
--
Bob Sankofa
fotobaraza.ning.com

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad