HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 14, 2026

SERIKALI GEITA YAAHIDI KUENDELEZA MAZINGIRA WEZESHI KWA VIJANA WENYE VIPAJI - DC MURAGILI

Serikali mkoani Geita imeahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana wenye vipaji vya michezo, hususan soka, ili kuwawezesha kuendeleza vipaji vyao na kufikia hatua ya kushiriki katika mashindano makubwa ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Muragili, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, wakati wa fainali ya michuano ya KNK CUP 2026, iliyofanyika katika dimba la Bukombe Stadium.

Katika fainali hiyo, Ushirombo Warriors waliibuka mabingwa baada ya kuifunga Katome FC kwa mabao 2–0.

Michuano ya KNK CUP ilianzishwa na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, ikiwa na lengo la kutoa jukwaa la kuibua na kukuza vipaji vya vijana kupitia mchezo wa soka.

Tangu kuanzishwa kwake, KNK CUP imeendelea kukua na kuwa sehemu muhimu ya kukuza na kuendeleza michezo katika Wilaya ya Bukombe.

Akisoma taarifa ya michuano hiyo kwa niaba ya Kamati ya Mashindano, Jenifer Kisusi amesema KNK CUP imekuwa na mchango mkubwa katika kuibua vipaji vya vijana.

Amesema mafanikio hayo yanaonekana pia kupitia vijana sita kutoka Bukombe waliofanikiwa kupata nafasi ya kuwa sehemu ya Timu ya Taifa iliyoshiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati mwaka 2026.

Kisusi amesema hatua hiyo ni ishara ya namna michuano hiyo inavyoendelea kutoa fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao na kupata nafasi za kushiriki katika ngazi za juu za soka.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad