Na Mwandishi Wetu,Kigoma
Kampuni ya tumbaku ya Alliance One Tanzania Tobacco Limited imepongezwa kwa kutoa mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira mkoani Kigoma kupitia katika miradi ya kurejesha uoto wa miti katika maeneo yaliyoathiriwa na shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabia nchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2026 Bw.Wazo Mwang’onda, baada ya kukagua mradi wa shamba la miti katika shule ya sekondari Munagana linalofadhiliwa na kampuni hiyo kwa kupanda miti ekari 414 ambapo mpaka sasa gharama za uendeshaji kwenye shamba hilo ni Shilingi 1,264,723,200.
Bw. Mwang’onda amebainisha kuwa kitendo cha kampuni ya Alliance One kuamua kuwekeza katika upandaji wa miti ni cha kizalendo na chenye nia ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhifadhi mazingira na kukuza Uchumi wa wananchi kupitia kilimo cha tumbaku na miti.
Mwang’onda ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Alliance One kuendelea kutoa usaidizi wa ujuzi kwa halmshauri za wilaya mkoani Kigoma pamoja na kuwajengea uwezo wananchi ili nao waanzishe mashamba yao na kukabailiana na jangwa ambalo linadhihirika kwa maeneo mengi ya wilaya ya Buhigwe kwa kutokuwa na miti, huku ardhi ya wilaya hiyo ikiruhusu kilimo cha miti ya mbao na mataunda.
“Nawapongeza kampuni ya Alliance One kwa juhudi kubwa mnayofanya katika mikoa mingi nchini Tanzania kwa kuanzisha na kuendeleza mashamba ya miti ikiwa ni sambamba na kuwapa hamasa na ujuzi wananchi katika sekita ya kilimo na mazingira, wito wangu kwenu sasa anzeni kuwahamasisha na kuwafundisha wananchi kupanda miti ya matunda hususani Parachichi ili pamoja na kuwapa kuni wapate matunda ambayo sasa yana soko kubwa kimataifa,”amesema.
Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge Kitaifa amesisitiza kuwa ardhi ya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma inafanana na maeneo mengi ya mkoa wa Njombe na Ruvuma, ambako pamoja na kupanda miti ya mbao, wananchi wamehamasishwa kuanzisha mashamba makubwa ya Parachichi na wakulima walioitikia wito huo sasa hivi uchumi wao umebadilika sana.
Akitoa taarifa ya miradi shirikishi ya mazingira inayotekelezwa na kampuni ya Alliance One, Meneja wa Kanda ya magharibi Bw. Salum Rashid amesema Mpango huo ulianza katika Mwaka wa Kilimo 2022/23 huko Ngukumo, Nzega, mkoani Tabora na baadaye Kasulu na Buhigwe mkoani Kigoma katika Mwaka wa Kilimo 2024.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa miradi ya uoteshaji na upandaji wa miti huanza kwa kusaini makubaliano kati ya AOTTL na mmiliki wa ardhi aliye tayari kushiriki katika uanzishaji wa shamba la miti, kwa lengo la kutoa nishati endelevu kwa wakulima wa tumbaku.
Tangu mwaka 2024 hadi sasa, kampuni imeanzisha shamba la miti lenye ukubwa wa hekta 966 sawa na takriban miti 2,415,675 katika Mkoa wa Kigoma, kati ya hiyo, hekta 414 zimepandwa katika eneo la wilaya ya Buhigwe, zikiwakilisha miti 1,035,000.
Kwa upande wake Mratibu wa shughuli za Alliance One mkoani Kigoma Bw. Robert Mogella ameweka bayana kuwa gharama za uendeshaji kwa ajili ya kusimamia hekta 414 zilizopandwa katika eneo la shule ya sekondari Munagana Songambele kwa kipindi cha miaka miwili ya kilimo ni TZS 1,264,723,200.
Bw. Mogella ameeleza kuwa pamoja na malengo mengine ya kukabiliana matumizi ya misitu asilia kwa ajili ya kuni za kukaushia tumbaku, kampuni hiyo ina malengo ya kuhamasisha jamii kuwekeza katika upandaji miti kwenye ardhi iliyoharibika ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkuu wa wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Kanali Michael Ngayalina akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa amebainisha kuwa Kampui ya Alliance One (AOTTL) imetoa mchango mkubwa kwa serikali na imekuwa chachu kwa wananchi kuanza kuthamini ardhi iliyokuwa imetelekezwa na sasa jamii inapanda miti katika mashamba yao.
Naye afisa Mazingira wa wilaya hiyo Bi. Asha Athuman Luhuyi ameweka bayana kuwa AOTTL ni mdau muhimu katika sekta ya mazingira wilayani Buhigwe, na kwamba kampuni hiyo imeiwezesha wilaya kuvuka hiyo lengo la upandaji miti milioni moja na laki tano kwa mwaka.
Mwenge wa Uhuru umeanza mbio zake leo Septemba 11, 2026 katika Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, ukitokea Wilaya ya Kasulu, ambapo unatarajiwa kuzindua, kutembelea, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akisoma taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mganasha wilayani Buhigwe, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Michael Ngayalina, amesema Mwenge huo utakimbizwa umbali wa kilomita 54 na kuzindua na kutembelea jumla ya miradi 7 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 15.4 ikiwemo inayosimamiwa na Kampui ya Alliance One Tobacco Tanzania Limited.
Kiongozi wa mbio za Mwenge Bw. Wazo Mwang’onda akiongea wakati Mwenge huo ulipotembelea shamba ya miti la ekari 414, lililopandwa kwenye shamba la shule ya sekondari Munagana,Wilayani Buhigwe,Mkoani Kigoma kwa ufadhili wa Kampuni ya Alliance One kwa gharama ya sh.Bilioni 1.2.
Meneja wa Upandaji Miti wa Kanda ya Magharibi wa Kampuni ya Alliance One, Bw Salum Rashid (wa nne kushoto) akiwa na wafanyakazi wenzake wakiwa wanaupokea Mwenge wa Uhuru(haupo pichani) ulipotembelea shamba la miti lililopo shule ya sekondari Munagana,wilayani Buhigwe,mkoani Kigoma lililofadhiliwa na kampuni hiyo




.jpeg)



No comments:
Post a Comment