Na Mwandishi Wetu, Tanga
TAASISI ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) imeondoa matumizi ya karatasi kwa wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo sehemu za kazi (field) katika ofisi na taasisi mbalimbali nchini na kuanza kutumia mfumo wa kidijitali wa kusimamia mafunzo hayo unaotambulika kama LST e-FIELD MIS 2026.
Hatua hiyo inalenga kurahisisha usimamizi wa mafunzo kwa vitendo sehemu za kazi pamoja na kuwawezesha wanafunzi kuwasilisha taarifa zao za mafunzo kwa njia ya kidijitali bila kulazimika kukutana ana kwa ana na wakufunzi wao.
Akizungumza katika maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea jijini Tanga, mkufunzi kutoka LST Bw. Khery Sanga amesema mfumo huo umeondoa vikwazo vilivyokuwa vikimkabili mwanafunzi katika kuwasilisha taarifa zake kwa mkufunzi anayemsimamia.
Amesema kupitia mfumo huo, mwanafunzi huweza kuingiza taarifa za mafunzo yake kila siku moja kwa moja kwenye mfumo, na mkufunzi huweza kuziona na kuzifanyia tathmini.
“Endapo mwanafunzi ataandika taarifa zake katika mfumo na mkufunzi asiridhie, mkufunzi huyo anapaswa kueleza kwenye mfumo sababu ya kutoridhia taarifa hizo” amebainisha.
Aidha ameongeza kuwa mfumo huo unamwezesha mwanafunzi kufanya mawasiliano na kuwasilisha taarifa za mafunzo kwa kutumia simu janja au kompyuta akiwa mahali popote.
Pia mfumo huo unawasaidia wakufunzi kuzipitia kazi wanazofanya wanafunzi wao kila siku wawapo kwenye mafunzo sehemu za kazi.
Sanga amefafanua kuwa LST hutoa mafunzo ya sheria kwa vitendo kwa kipindi cha mwaka mmoja; ambapo katika miezi sita ya kwanza mwanafunzi hujifunza kwa vitendo akiwa darasani, na baada ya hapo huendelea na mafunzo ya vitendo akiwa sehemu za kazi kwa kipindi kingine cha miezi sita.
Sanga ametoa msisitizo kwa wanafunzi wa LST kutumia kikamilifu mfumo huo wa kidijitali ili uweze kuwasaidia kutunza na kuwasilisha taarifa zao kwa ufanisi na hatimaye kuwawezesha kufikia malengo ya mafunzo yao.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment