Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JUMUIYA ya Khoja Shia Ithnasheri Mkoa wa Dar es Salaam, kupitia taasisi zake, imeanza kutoa huduma mbalimbali za afya na macho bure kwa wananchi katika Kambi ya siku tatu ya Mafunzo ya Imam Hussein (a.s), inayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Kambi hiyo imeandaliwa ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya kifo cha mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W), Imam Hussein (a.s), kilichotokea Karbala nchini Iraq zaidi ya miaka 1,400 iliyopita.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Mohammed Razzadewji, amesema maisha na mafundisho ya Imam Hussein yanasisitiza kujitolea kwa ajili ya jamii bila kubagua watu kwa misingi ya dini, kabila au jinsia.
Amesema Imam Hussein (a.s) alijitoa katika kuupigania umma wa babu yake, Mtume Muhammad (S.A.W), jambo ambalo linapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
Katika kambi hiyo, wananchi wamepatiwa huduma mbalimbali za afya, zikiwemo upimaji wa macho, shinikizo la damu, kisukari, saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti kwa wanawake, pamoja na uchunguzi wa tezi dume kwa wanaume.
Huduma nyingine zilizotolewa ni elimu kuhusu afya ya akili na uchangiaji wa damu salama, huku wananchi wakipata fursa ya kupata elimu kuhusu umuhimu wa kufahamu hali zao za kiafya.
Akizungumzia kambi hiyo, Alhaj Mohammedraza Dewji amesema kujitolea kwa ajili ya jamii ni sehemu ya misingi inayopaswa kuishi nayo kila mwanadamu, akirejea mfano wa Imam Hussein ambaye, kwa mujibu wa mafundisho hayo, alijitoa kwa ajili ya kulinda kizazi cha babu yake.
Amesema mwamko wa wananchi katika kambi hiyo umeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita, ambapo kwa siku kambi hiyo ina uwezo wa kuhudumia hadi wagonjwa 2,000.
“Katika kambi ya safari hii kulikuwa na utofauti na mwaka jana. Wagonjwa wote waliokutwa na changamoto ya mtoto wa jicho walipelekwa moja kwa moja katika moja ya hospitali zetu, Medwell iliyopo Kibaha, Mkoa wa Pwani, na kwa wengine walipangiwa siku ya kwenda kupata matibabu katika hospitali zetu za Medwell na KSIJ Charitable Eye Centre iliyopo Temeke,” alisema Mohammedraza.
Amesema idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kupata huduma ni ishara ya mwamko mkubwa wa jamii kuhusu afya, huku akibainisha kuwa baadhi ya wananchi waligundulika kuwa na matatizo mbalimbali ambayo hawakuwa wakiyafahamu.
Kwa mujibu wa Mohammedraza, baadhi ya wananchi waligundulika kuwa na mtoto wa jicho, wengine uono hafifu na kupewa miwani, huku wengine wakipewa dawa za kutibu matatizo ya macho. Pia, wananchi walifanyiwa vipimo vya magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo shinikizo la damu.
Amesema Jumuiya hiyo ilishirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Kitengo cha Damu Salama pamoja na Taasisi ya Saratani Ocean Road katika kutoa huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi kwa wanawake.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kujenga utamaduni wa kuchangia damu salama, akisema damu hiyo inahitajika katika hospitali mbalimbali, hususani kwa wanawake wajawazito na waathirika wa ajali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Madaktari katika Kambi hiyo ya Afya na Macho, Dkt. Noushad Bandali, amesema uchangiaji wa damu ni huduma ya kujitolea ambayo inapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wa kila mtu mwenye sifa ya kuchangia damu.
Dkt. Bandali amesema mahitaji ya damu katika hospitali ni makubwa, hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza mara kwa mara kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa.
Aidha, amesema kambi hiyo imetoa elimu kuhusu afya ya akili, eneo ambalo amesema bado halipatiwi uzito unaostahili katika jamii licha ya kuongezeka kwa changamoto zinazohusiana na afya ya akili, ikiwemo msongo wa mawazo.
Mmoja wa wanufaika wa kambi hiyo, Mariam Akida, mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam, amesema amefaidika kwa kupata matibabu ya mtoto wa jicho baada ya kukabiliwa na tatizo la uono hafifu kwa muda mrefu bila kujua chanzo chake.
Amesema utaratibu uliowekwa na waandaaji wa kambi hiyo umekuwa mzuri kwa kuwa wananchi wamekuwa wakielekezwa katika maeneo mbalimbali ya huduma, hivyo kupunguza muda wa kusubiri.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kambi hiyo kutoka Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri Mkoa wa Dar es Salaam, Jahmeed Kassam, amesema wananchi wote watakaofika katika kambi hiyo ya siku tatu watahudumiwa na timu ya wawezeshaji na wataalamu wapatao 500 waliopo katika viwanja hivyo.
Kambi hiyo imehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa dini, Serikali na siasa, huku wananchi wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam wakijitokeza kwa wingi kupata huduma za afya na kushiriki katika mafunzo kuhusu maisha na mafundisho ya Imam Hussein (a.s).


No comments:
Post a Comment