HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, August 15, 2026

GGML Yarejesha Matumaini kwa Watoto 300

 




Na Mwandishi Wetu.
GEITA Gold Mining Limited (GGML) imetenga takribani Sh bilioni 1.2 kwa kipindi cha miaka mitatu kusaidia matibabu ya watoto 300 wenye magonjwa ya moyo nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa watoto ambao familia zao zinaweza kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Kupitia makubaliano yaliyosainiwa leo katika ofisi za makao makuu ya GGML mkoani Geita, kati ya kampuni hiyo na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), GGML itatoa takribani Sh milioni 400 kila mwaka kusaidia matibabu ya watoto 100 wenye matatizo ya moyo, hivyo kufikisha jumla ya watoto 300 ndani ya miaka mitatu. Ushirikiano huo umefikiwa kwa uratibu wa Global Medicare ya jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat, amesema uamuzi wa kampuni kuunga mkono mpango huo ulifikiwa baada ya kupitia mchakato wa kina wa tathmini unaotumika katika miradi yote ambayo kampuni inaombwa kuisaidia.

“Tunatazamia ushirikiano wa miaka mitatu. Ni watoto 100 kwa mwaka na takribani Sh milioni 400 kwa mwaka. Tunatarajia ushirikiano huu kuwa wa mafanikio na tunatumaini utaendelea hata katika siku zijazo,” amesema Suryaningrat.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dkt. Peter Kisenge, amesema msaada huo una umuhimu mkubwa kwa sababu utagusa moja kwa moja maisha ya watoto wanaohitaji huduma za haraka za moyo, wakiwemo wanaohitaji upasuaji na taratibu maalumu za kuziba matundu ya moyo.

“Huu si msaada wa pesa tu. Huu ni msaada unaokwenda kuokoa maisha. Mmeenda kutimiza matumaini ya watoto ambao wanakwenda kujenga Taifa la Tanzania la kesho,” amesema Dkt. Kisenge.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Global Medicare, Abdulmalik Mollel, amesema magonjwa ya moyo yanaendelea kuwa changamoto kubwa, huku JKCI ikiwa imejijengea nafasi muhimu katika utoaji wa huduma za kibingwa za moyo kwa Watanzania pamoja na wagonjwa kutoka nchi nyingine za ukanda huu, ikiwemo Zambia, Malawi, Kenya na Uganda.

Mollel amesema uamuzi wa GGML kutoa mchango huo ni hatua kubwa katika kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo na unadhihirisha namna sekta binafsi inaweza kushirikiana na taasisi za Serikali katika kuokoa maisha.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad