Na Mwandishi Wetu
TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imesema Serikali imeanza maandalizi ya kuanzisha mpango wa kuzalisha umeme wa nyuklia, huku ikisisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo utafuata kikamilifu viwango vya kimataifa vya usalama ili kulinda wananchi, mazingira na kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la TAEC kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat Kassim Mohammed, amesema Tanzania ipo katika hatua za awali za maandalizi kabla ya kuingia rasmi katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo.
Alisema Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa kisheria, sera na taasisi zitakazosimamia matumizi ya teknolojia ya nyuklia ili kuhakikisha uzalishaji wa umeme unafanyika kwa kuzingatia viwango vya usalama vinavyokubalika kimataifa, sambamba na kujenga uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati hiyo.
Prof. Najat alisema TAEC tayari imewaalika wataalamu wa kimataifa kufanya tathmini ya utayari wa Tanzania katika kutekeleza mpango huo.
Alieleza kuwa endapo tathmini hiyo itaridhisha, nchi itapata kibali cha kuendelea na hatua inayofuata ya utekelezaji.
Aidha, alisema Serikali inalenga ndani ya kipindi cha miaka saba kuanza kuzalisha umeme wa nyuklia, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika, kuimarisha ukuaji wa uchumi na kuchochea maendeleo ya sekta ya viwanda.
Akizungumzia upatikanaji wa malighafi, Prof. Najat amesema Tanzania ina akiba ya madini ya Urani, ambayo ndiyo malighafi muhimu katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia kuongeza kuwa madini ya urani lazima yachakatwe kwa teknolojia maalumu kabla ya kutumika kama mafuta ya nyuklia.
Alieleza kuwa katika hatua za mwanzo, urani itakayochimbwa nchini itasafirishwa kwenda nje ya nchi, ikiwemo Urusi, kwa ajili ya kuchakatwa, kisha kurejeshwa Tanzania kwa matumizi ya kuzalisha umeme.
Prof. Najat alisema mradi wa uchimbaji wa madini ya urani unatarajiwa kuanza katika eneo la Mkuju, mkoani Ruvuma, huku shughuli za utafiti zikiendelea katika maeneo mengine ili kubaini akiba zaidi zenye uwezo wa kuchimbwa kibiashara.
Pamoja na hayo, aliwataka wananchi kujenga uelewa sahihi kuhusu teknolojia ya nyuklia na kuondoa hofu zisizo na msingi, akisisitiza kuwa Serikali inatekeleza mpango huo kwa kuzingatia miongozo na viwango vya kimataifa vinavyolenga kuhakikisha usalama wa watu, mazingira na miundombinu.
Alisema matumizi ya teknolojia ya nyuklia yana mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa, siyo tu katika uzalishaji wa umeme, bali pia katika sekta za afya, kilimo, viwanda na utafiti wa kisayansi.

.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment