HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 6, 2026

Airtel Yaweka Alama Ruaha Marathon: Yabeba Agenda ya Mazingira na Ustawi wa Wafanyakazi

 

Na Mwandishi Wetu, Iringa
KAMOUNI ya mawasiliano ya Airtel Tanzania imeendelea kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya jamii kwa kuunganisha ajenda za afya, ustawi wa wafanyakazi na uhifadhi wa mazingira kupitia udhamini wake wa mbio za ‘Great Ruaha Marathon 2026’, zilizofanyika hivi karibuni ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Ikiwa Mdhamini Rasmi kutoka sekta ya Mawasiliano, Airtel ilishiriki pamoja na mamia ya wakimbiaji katika tukio ambalo limeendelea kujijengea sifa kama moja ya mbio za kipekee nchini zinazochanganya michezo, utalii na juhudi za kuhifadhi mfumo wa ikolojia wa Mto Mkuu wa Ruaha.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo mkoani Iringa, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Airtel Tanzania, Bi. Stellah Kibaja, alisema ushiriki wa kampuni hiyo unaonyesha dhamira yake ya kuleta mchango chanya kwa jamii, hatua inayokwenda sambamba na shughuli zake za kibiashara.

"Airtel tunaamini kuwa mahusiano imara hayajengwi kupitia mtandao wetu pekee, bali kupitia watu, uzoefu wa pamoja na jamii zinazounganishwa na lengo moja. Ndiyo maana tunajivunia kuwa sehemu ya Great Ruaha Marathon, tukio linaloendana na maadili yetu ya kuhamasisha afya bora, kuunga mkono jamii na kushiriki katika mipango yenye manufaa ya kudumu," alisema Bi. Kibaja.

Katika kuonyesha mfano wa uongozi unaoshiriki kwa vitendo, Airtel iliwashirikisha wafanyakazi 20 katika mbio hizo, wakiwemo wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji ya kampuni hiyo.

Bi. Kibaja alibainisha kuwa kampuni hiyo inaamini afya ya wafanyakazi ndio msingi mkuu wa mafanikio ya taasisi yoyote inayotaka kupiga hatua.

"Watu wenye afya hujenga timu imara, timu imara hujenga biashara zenye mafanikio, na biashara zenye mafanikio huchangia zaidi maendeleo ya jamii. Uongozi hauonekani kwenye vikao pekee, bali pia katika kushiriki bega kwa bega na wafanyakazi na kuhamasisha wengine kupitia matendo," alisisitiza.

Aliongeza kuwa Airtel imeendelea kuwekeza katika programu za ustawi wa wafanyakazi zinazolenga kuimarisha afya ya mwili, akili na uwiano kati ya kazi na maisha binafsi, hatua inayosaidia kuongeza tija kazini na kuboresha huduma kwa wateja.

Mbali na michezo, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa Airtel inaunganisha mamilioni ya Watanzania kila siku kupitia huduma za sauti, intaneti, intaneti ya nyumbani (Airtel Smart Box) na Airtel Money, huku ikizidi kupanua mtandao wake hadi vijijini.

"Mawasiliano ni zaidi ya kuunganisha watu; ni kufungua fursa. Iwe ni mwanafunzi anayesoma mtandaoni, mkulima anayepokea malipo kupitia Airtel Money, au mfanyabiashara anayekuza biashara yake kidijitali, kila muunganisho una nafasi ya kuboresha maisha ya Watanzania," alisema.

Akifunga maelezo yake kabla ya kuanza kwa mbio hizo, Bi. Kibaja aliwataka washiriki kuona mbio hizo kama jukwaa la kipekee la kuleta mabadiliko.

"Haijalishi unamaliza wa kwanza au wa mwisho. Kilicho muhimu ni kwamba umechagua kuwekeza katika afya yako, kuunga mkono uhifadhi wa mazingira na kuwa sehemu ya harakati zinazozalisha mabadiliko chanya kwa jamii," alihitimisha.

Mbio za Great Ruaha Marathon zimeendelea kukua na kuwa jukwaa muhimu linalovutia ushiriki wa sekta binafsi nchini katika kuhamasisha afya, kukuza utalii endelevu, na kuimarisha uhifadhi wa ikolojia ya Mto Mkuu wa Ruaha ambao ni uti wa mgongo wa hifadhi hiyo na nishati nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad