HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 23, 2026

POLISI ARUSHA WAFUNGUA MILANGO YA AJIRA KWA VIJANA WA MAZINGIRA MAGUMU



Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi

NDOTO za vijana wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Arusha zimeanza kupata mwanga baada ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo, kuzindua mpango wa kuwabaini na kuwapa mafunzo ya udereva bila malipo kwa kushrikiana na vyuo vya udereva, hatua inayolenga kuwajengea ujuzi na kuwainua kiuchumi.

Akizungumza mara baada ya kufungua mafunzo hayo leo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani humo, ACP Zauda Mohamed amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha vijana, ili kuwaondoa kwenye mazingira magumu yanayoweza kuwashawishi kujihusisha na vitendo vya kihalifu kwa kuwapatia ujuzi utakaowajengea uwezo wa kujitegemea.

ACP Zauda amebainisha kuwa, vijana hao waliwachukua kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo vituo vya kulelea watoto wenye changamoto za malezi, maeneo ya kuegesha na kuosha magari, wanaobeba mizigo sokoni pamoja na wapiga debe katika vituo vya mabasi.

Aidha, amefafanua kuwa pamoja na kugharamia mafunzo hayo, Jeshi hilo pia litahakikisha linawasimamia vijana hao katika hatua zote za kupata leseni za udereva ili kuongeza fursa zao za kujiajiri au kuajiriwa mara baada ya kuhitimu mafunzo.

Mkuu huyo wa usalama barabarani amemaliza kwa kusema kuwa, anaamini kuwa baada ya vijana hao kuhitimu na kupata leseni zao za udereva, itakuwa ni chachu ya mabadiliko kwao kiuchumi, kuwaondoa katika makundi hatarishi lakini poa kuwaepusha na uhalifu.

Naye Bw. Godfrey Laizer, mnufaika wa mafunzo hayo anayejishughulisha na kubeba mizigo amesema mafunzo hayo yamempa matumaini mapya, akieleza kuwa yatamwezesha kupata leseni ya udereva na kufungua fursa za ajira pamoja na kuboresha maisha yake.

Kijana kutoka kituo cha kulelea watoto yatima cha Kindness Children Care, Bw. Steven Daniel amelishukuru Jeshi la Polisi kwa fursa hiyo, akisema watajituma katika mafunzo ili kutimiza ndoto zao za badaye.

Kwa upande wake Bi. Emmy Frank anayejishughulisha na kuosha magari amesema mafunzo hayo yatamjengea ujuzi na kumpa nafasi ya kupata ajira zenye kipato bora. Ameahidi kuitumia vyema fursa hiyo na kuzingatia mafunzo yote atakayopatiwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad