WANANCHI wa Jimbo la Monduli wamempokea kwa shangwe Mlezi wao wa Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) na kutuma salamu kuwa wako bega kwa bega na Serikalini katika kuleta maendeleo nchini.
Salamu hizo zimetolewa tarehe 23 Julai 2026 wakati wa mkutano wa hadhara wa Mhe. Waziri Chongolo na maelfu ya wananchi waliojikusanya katika eneo la Soko la Losirwa, Kata ya Esilalei, Wilaya ya Monduli.
“Hongereni kwa kujibiidiisha kwa kazi. Nimepokea kilio chenu cha kujengewa soko la kisasa la Losirwa, niwahakikishie Wizara itafanyia kazi hilo; sambamba na kukamilisha ukarabati wa skimu ya umwagiliaji ya Mto wa Mbu kwa gharama ya shilingi bilioni 17 chini ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili kutatua matatizo ya kilimo cha umwagiliaji katika Kata za Wilaya ya Monduli,” amesema Mhe. Chongolo.
Akizungumza kwa niaba yao, Mbunge wa Jimbo la Monduli Mhe. Joseph İsack Copiriano amesema kuwa wananchi wa Monduli wanaipongeza Serikali kwa kusogeza huduma za kijamii na kupeleka miradi ya maendeleo ikiwemo elimu, afya na kilimo.
“Kilio chao ni mbolea ipatikane, wanahitaji maji na ujenzi wa barabara, ikiwa ni pamoja na kupata elimu zaidi kuhusu kilimo cha malisho ya mifugo,” ameeleza Mhe. Copiriano.
Akijibu hoja za wananchi, Mhe. Chongolo ameahidi kuwa zitafanyiwa kazi na Wizara ya Kilimo na Taasisi zake, huku akisisitiza kwa wananchi umuhimu wa kulinda miundombinu na vyanzo vya maji kwa kuwa mabwawa madogo yanaweza kujengwa maeneo hayo kwa ajili ya shughuli za kilimo na kunywesha mifugo.
Katika nyakati tofauti, Waziri Chongolo pia ametembelea Shule ya Sekondari ya Manyara yenye wanafunzi zaidi 1,800 na kuzindua bweni la wanafunzi wavulana.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

No comments:
Post a Comment