HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 24, 2026

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga lawafariji wagonjwa




Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga limetekeleza matendo ya huruma kwa kutembelea na kuwafariji wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Kambarage, kilichopo Manispaa ya Shinyanga, huku likitoa ujumbe wa matumaini, maadili na usalama kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Fraterine Tesha amesema Jeshi la Polisi linatambua kuwa wagonjwa ni sehemu ya jamii inayolihudumia na kulilinda, hivyo limeona ni muhimu kufika kituoni hapo kuwapa pole na kuwatia moyo.

ACP Tesha, amewaasa wagonjwa kuwa na uvumilivu wakati wa matibabu, akisisitiza kuwa jamii inaendelea kuwaombea ili wapone na kurejea katika shughuli zao za kila siku za kushiriki ujenzi wa Taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Shinyanga, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Zainabu Mangara, amewapongeza wanawake waliojifungua katika kituo hicho cha afya na kuwakumbusha umuhimu wa kulea watoto wao katika misingi ya maadili mema.

ASP Mangara, ametoa elimu ya usalama barabarani kwa wazazi hao, akiwakumbusha kutowaruhusu watoto wao kupandishwa kwenye pikipiki zaidi ya mtoto mmoja kwa wakati mmoja, akieleza kuwa kitendo hicho kinaongeza hatari ya ajali na kuhatarisha maisha ya watoto pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Kituo hicho, Mganga Mfawidhi Dkt. Ernest Kurwa amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kutenga muda wa kutembelea na kuwafariji wagonjwa.

Dkt. Kurwa amesema ziara za aina hiyo huwapa wagonjwa faraja na matumaini, huku akitoa wito kwa jamii kujenga utamaduni wa kutembelea wagonjwa hospitalini ili kuwapa moyo na kuwafanya wajione kuwa hawapo peke yao katika kipindi cha changamoto za kiafya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad