HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, July 4, 2026

JKT Yaibuka tena Mshindi wa Kwanza wa Bidhaa za Kilimo na Uvuvi Kwenye Maonesho ya 50 (Sabasaba)

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Sabasaba Kitaifa upande wa JKT, Brigedia Jenerali Shija Lupi akizungumza waandishi wa habari kuhusiana na JKT kuibuka mshindi wa Kwanza katika Bidhaa za Kilimo na Uvuvi kwenye Maonesho ya 50  Biashara ya Biashara Kimataifa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Sabasaba Kitaifa upande wa JKT, Brigedia Jenerali Shija Lupi, akiwa katika picha ya pamoja na maafande wa JKT  mara baada ya kushangilia ushindi wa ubunifu wa jeshi katika bidhaa za Kilimo na Uvuvi.

Na Mwandishi Wetu
JESHI  la Kujenga Taifa (JKT) limeibuka mshindi wa kwanza katika kundi la bidhaa za kilimo na uvuvi kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), mafanikio ambayo yameelezwa kuwa ni matokeo ya uzalishaji wenye ubora, ushirikiano na utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wa jeshi hilo.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Sabasaba Kitaifa upande wa JKT, Brigedia Jenerali Shija Lupi, alisema ushindi huo unathibitisha kuwa bidhaa zinazozalishwa na JKT zinakidhi viwango vya ushindani na zimeendelea kutambulika nchini.

Alisema tuzo hiyo si ya kwanza kwa JKT, kwani taasisi hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika maonesho hayo kwa miaka iliyopita kupitia bidhaa zinazozalishwa na Shirika la SUMA JKT.

"Hata mwaka jana tulikuwa washindi wa kwanza kwa bidhaa za samani na mwaka huu tumeamua kushindana katika kundi la bidhaa za kilimo na uvuvi na tumefanikiwa kuibuka washindi wa kwanza. Hii inatupa hamasa ya kuendelea kuboresha bidhaa zetu ili tuendelee kufanya vizuri kila mwaka," alisema.

Alisema ushirikiano uliopo katika mnyororo mzima wa uzalishaji umeiwezesha JKT kuendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora na ushindani mkubwa sokoni.

Akizungumzia mchango wa JKT katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Brigedia Jenerali Lupi alisema taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuzalisha chakula na mazao ya biashara pamoja na kutoa mafunzo kwa wananchi.

Alieleza kuwa JKT inamiliki mashamba makubwa ya uzalishaji na ranchi mbalimbali, ikiwemo Ranchi za Misenyi, Orujoro na Mafinga, huku ikiendelea na ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha uzalishaji wa maziwa kitakachoongeza thamani ya bidhaa za mifugo.

Aidha, alisema kupitia kampuni zake, ikiwemo SUMA JKT, taasisi hiyo imeendelea kuzalisha bidhaa mbalimbali za viwandani pamoja na kutoa huduma za kitaalamu katika sekta ya kilimo na uvuvi.

Alitaja pia mchango wa kampuni ya SUMA Poni, inayojihusisha na ujenzi wa mabwawa ya kisasa ya ufugaji wa samaki na usimikaji wa mifumo ya uzalishaji, huku wataalamu wa JKT wakiendelea kutoa ushauri wa kitaalamu bila malipo kwa wananchi wanaohitaji kuwekeza katika kilimo, mifugo na uvuvi.

Brigedia Jenerali Lupi aliwataka wananchi kutembelea banda la JKT katika Maonesho ya Sabasaba ili kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na taasisi hiyo pamoja na kupata elimu kuhusu fursa za uzalishaji na uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad