HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 12, 2026

Tanzania yajipanga kunufaika na gesi trilioni 57.54

Mtwara. Tanzania imeingia katika hatua mpya ya maendeleo ya sekta ya gesi asilia kufuatia kuthibitishwa kwa uwepo wa akiba kubwa inayokadiriwa kufikia futi trilioni 57.54, hatua inayotarajiwa kubadilisha mwelekeo wa uchumi wa Taifa.

Ugunduzi wa rasilimali hiyo inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye fursa kubwa zaidi za uwekezaji katika nishati barani Afrika.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Juni 12, 2026 wakati Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) pamoja na kamati zake walipotembelea miradi ya gesi asilia katika eneo la Mnazi bay, mkoani Mtwara kwa lengo la kujifunza na kujionea maendeleo ya shughuli za utafutaji, uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni, amesema gesi hiyo hutumika kwa takribani asilimia 35 kwa ajili ya kuzalisha umeme unaotumika hapa nchini.


Ameeleza kuwa, maeneo yote yaliyogunduliwa kuwa na gesi asilia yanaendelea kufanyiwa kazi ili rasilimali hiyo iweze kuzalishwa na kutumika kwa manufaa ya taifa.

“Sasa tukaona ni vema kuongeza idadi ya visima ili kuongeza uzalishaji wa gesi asilia. Gesi nyingi huzalishwa na kupelekwa katika mitambo ya Madimba inayomilikiwa na TPDC, ambako hutumika kuzalisha umeme,” alisema Sangweni.

Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi wa Petroli wa PURA, Fabian Mwose, alieleza hatua za awali za utafutaji wa gesi asilia katika visima vitatu vipya vilivyopo eneo la Mnazi Bay.

Alisema kisima cha Kasa, ambacho ni cha tatu katika kampeni ya uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia, kilianza kutobolewa Juni 1, 2026, na kinatarajiwa kuchukua takribani siku 55 kukamilika.

Mwose alisema baada ya uchimbaji kukamilika, tathmini na maandalizi ya uzalishaji yatafanyika endapo uwepo wa gesi asilia utathibitishwa katika kisima hicho.

“Kwa mujibu wa tafiti za awali zilizofanyika, kisima hicho kinakadiriwa kuwa na takribani futi za ujazo bilioni 167 za gesi asilia, ambazo zinaweza kuzalishwa kwa wastani wa futi za ujazo milioni 35 kwa siku,” alisema Mwose.

Aliongeza kuwa uzalishaji wa gesi kutoka katika kisima hicho utaongeza kiwango cha gesi asilia kinachozalishwa nchini, jambo litakalosaidia kukidhi mahitaji ya nishati katika sekta mbalimbali, hususan viwandani. 

Alisema hatua hiyo pia itachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania kupitia maendeleo ya viwanda vinavyotegemea gesi asilia.

Mwenyekiti wa Bodi ya PURA, Halfani Halfani, amesema ziara hiyo imewapa fursa ya kuelewa kwa undani mchakato wa utafutaji, uchimbaji na uzalishaji wa gesi asilia nchini.

Aliongeza kuwa wananchi, hususan wa Mkoa wa Mtwara, wanaendelea kunufaika na uwekezaji katika sekta hiyo kupitia ongezeko la shughuli za kiuchumi, mzunguko wa fedha pamoja na maendeleo ya miundombinu kama barabara na huduma nyingine za kijamii.

Katika ziara hiyo, wajumbe walitembelea kisima cha utafutaji wa gesi asilia cha Kasa kilichopo Mnazi Bay pamoja na Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad