*Waumini Wahamasishwa Kuchangia Ujenzi wa Makao Makuu ya EMCT Kyela
Na Mwandishi Wetu
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Moravian Tanzania (EMCT), Joseph Mwambungu, amewataka Watanzania kuendelea kuhubiri na kuishi katika imani ya Mungu ili kuimarisha maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii.
Akizungumza wakati wa ibada ya Jumapili katika Usharika wa Mburahati jijini Dar es Salaam, Askofu Mwambungu alisema hakuna mtu anayeweza kufanikiwa kwa uwezo wake mwenyewe bila kumtegemea Mungu katika maisha yake ya kila siku.
Alisema baadhi ya changamoto zinazowakabili watu hutokana na kuishi maisha yanayomweka Mungu pembeni, huku akisisitiza umuhimu wa kurejea katika misingi ya imani, maadili na uadilifu ili kujenga taifa lenye maendeleo endelevu.
Askofu Mwambungu alieleza kuwa Tanzania imeendelea kujulikana duniani kwa kudumisha amani na utulivu, hivyo wananchi wote wana wajibu wa kuilinda na kuiendeleza kwa nguvu zao zote. Alibainisha kuwa moja ya majukumu makubwa ya kanisa ni kuendelea kuiombea nchi ili amani iendelee kudumu.
“Amani ikitoweka hata ibada haziwezi kufanyika kwa utulivu na maendeleo hayawezi kupatikana. Ni amani inayowezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za kijamii na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo,” alisema.
Aidha, aliwataka waumini na wananchi kwa ujumla kuwaombea viongozi wa nchi ili mipango na maamuzi wanayoyafanya yaweze kufanikiwa kwa manufaa ya taifa na wananchi wake.
Katika hatua nyingine, Askofu Mwambungu aliwaalika waumini na wadau mbalimbali kushiriki katika kuchangia ujenzi wa Makao Makuu ya Kanisa la Kiinjili la Moravian Tanzania yanayojengwa Kyela mkoani Mbeya.
Alisema kukamilika kwa makao hayo kutaimarisha utoaji wa huduma za kiroho na kiutawala kwa kuwa yatawezesha idara mbalimbali za kanisa kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi katika kusimamia huduma za uchungaji na maendeleo ya kanisa.

.jpeg)

.jpeg)

No comments:
Post a Comment