HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 3, 2026

ALBINISM SPORTS CLUB NA TASACI WASHIRIKIANA KUANDAA MECHI YA KIRAFIKI NA TIMU YA BUNGE ITAKAYOCHEZWA JUNI 6

Na Mwandishi Wetu

ALBINISM Sports Club yenye Makao Makuu yake jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira
(TASACI), imeandaa mechi ya kirafiki kati ya timu ya Bunge.

Mechi hiyo ya kirafiki itakayofanyika Juni 6 2026 katika Uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma na mtanange huo huo ni sehemu ya maandalizi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa kuhusu Ualbino, ambayo huadhimishwa duniani kote Juni 13 Juni kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu haki, usawa, heshima na ustawi wa watu wenye ualbino.

Taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari leo Juni 3,2026 na Abdallah Majiwa ambaye ni 
Mwenyekiti wa Albinism Sports Club amesema tukio hilo linatarajiwa kuwakutanisha pamoja Wabunge, watu wenye ualbino, wananchi wa Jiji la Dodoma na maeneo ya jirani na wadau mbalimbali wa masuala ya
haki za binadamu. 

Amefafanua kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Wezesha Watu Wenye Ualbino kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu.” Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo.

“Tunatoa mwito kwa wananchi wote wa Dodoma na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki na kuunga mkono tukio hili muhimu lenye lengo la kujenga jamii yenye usawa, heshima na fursa
kwa wote.

“Mbali na burudani ya michezo, mechi hii inalenga kuhamasisha ushirikishwaji wa watu wenye ualbino katika nyanja zote za maendeleo, kuongeza uelewa wa jamii kuhusu changamoto na fursa zinazowakabili, na kuendeleza mjadala kuhusu haki, usawa na fursa kwa watu wenye ualbino nchini Tanzania.”

Ameongeza malengo mahsusi ya mechi hiyo ni kuwaleta pamoja Wabunge, watu wenye ualbino na wadau mbalimbali ili kujenga mshikamano na kutafakari kwa pamoja namna bora ya kuwalinda, kuwawezesha na kuwaendeleza watu wenye ualbino;

Pia kuunganisha juhudi za Bunge, Serikali na wadau wengine katika kupinga unyanyapaa,
kuondoa imani potofu, na kukomesha vitendo vya ubaguzi na ukatili dhidi ya watu wenye
ualbino,kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya yanayowahusu watu wenye ualbino hususan
umuhimu wa kinga dhidi ya miale ya jua na utunzaji wa afya ya ngozi;

Katika siku hiyo pia shughuli mbalimbali siku ya mechi ya waheshimiwa wabunge na watu wenye ualbino, inayotarajiwa kuanza saa 11 jioni na itatanguliwa na matukio mbalimbali muhimu yatakayolenga kuelimisha, kuhamasisha na kukuza ushirikishwaji wa watu wenye ualbino katika jamii. 

Amesema matukio hayo ni pamoja na semina kubwa kuhusu masuala ya afya, mazingira na haki za watu wenye ualbino, utoaji wa huduma za afya ya ngozi, uwasilishaji wa risala ya waandaaji, hotuba fupi kutoka kwa viongozi mbalimbali wakiwemo waheshimiwa wabunge na mgeni rasmi pamoja na uzinduzi rasmi wa Albinism International Marathon. 

Kuhusu Historia ya Siku ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa Juu ya Ualbino (13 Juni)
inatokana na Azimio la umoja wa mataifa kuhusu kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa kuhusu Ualbino (International Albinism Awareness Day) lilipitishwa Desemba 18 2014 kupitia Azimio Na. A/RES/69/170 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Aidha Juni 13 ilichaguliwa kuwa siku rasmi ya maadhimisho hayo kwa sababu ndio tarehe ambayo Umoja wa Mataifa ulipitisha Azimio lake la kwanza kuhusu haki za watu wenye ualbino mwaka 2013.

Kuhusu Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira amesema  ni mdau muhimu katika maadhimisho haya kupitia shughuli mbalimbali za elimu, afya na uhifadhi wa mazingira. 

Mchango wake unajumuisha kuelimisha jamii kuhusu afya ya ngozi, kinga dhidi ya madhara ya mionzi ya jua kwa watu wenye ualbino, pamoja na kupinga imani potofu zinazochochea unyanyapaa na ukatili.Pia kukuza matumizi sahihi na salama ya tiba asilia kwa mujibu wa Sheria Na. 23 ya mwaka 2002 ya Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Pia kuhamasisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira kama msingi wa afya bora ya jamii,kulinda mimea tiba na rasilimali nyingine za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
kijacho na kushirikiana katika kampeni za kupinga unyanyapaa, ubaguzi na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino na watu wenye ulemavu kwa ujumla kupitia michezo na shughuli za kijamii.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad