HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 3, 2026

TANZANIA GENERATION CARE YATOA MSAADA WA SARUJI, MABATI NA MATOFALI KWA MZEE LUPITA

 




Taasisi ya Tanzania Generation Care imetoa msaada wa mifuko ya saruji, mabati pamoja na matofali kwa ajili ya kumsaidia mlemavu wa macho, Mzee Paulo Lupita, mkazi wa Tabata Mawezi, Dar es Salaam, ambaye nyumba yake imebomoka na hivyo kulazimika kulala nje.


Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi msaada huo kwa Mzee Lupita, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Generation Care, Bi. Fauzia Mbwana, amesema taasisi hiyo imeguswa kumsaidia kutokana na hali yake ya uhitaji. 


Amesema Mzee Lupita pamoja na mke wake ni watu wenye ulemavu na wanahitaji msaada ili kuboresha maisha yao, hasa baada ya kulazimika kuishi nje kufuatia kubomoka kwa nyumba yao.


Bi. Mbwana amesema wanaamini msaada huo utasaidia kutatua changamoto inayowakabili kwa kuwezesha ujenzi wa sehemu ya nyumba ambayo ukuta wake ulianguka, hali iliyowalazimu kuishi bila makazi salama.


Aidha, amesema kuwa Taasisi ya Tanzania Generation Care imelenga kuboresha maisha ya jamii kwa kutoa elimu ya malezi kwa watoto pamoja na kusaidia watu wenye mahitaji maalum na makundi mengine yenye uhitaji.


"Lengo letu ni kujenga familia yenye elimu, afya na usawa. Katika kufikia malengo hayo, tunafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kuleta mabadiliko chanya na maendeleo endelevu," amesema Bi. Mbwana.


Bi. Mbwana pia ameshukuru kupata fursa ya kukutana na familia hiyo ili kutathmini namna bora ya kuwasaidia katika kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.


Kwa upande wake, Mzee Paulo Lupita ameishukuru Taasisi ya Tanzania Generation Care kwa msaada huo, akisema utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya makazi anayokumbana nayo.


 Aidha, amesisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kuwasaidia watu wenye uhitaji ili kuboresha maisha yao.







No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad