HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 2, 2026

BoT YASALIA NA RIBA YA MSINGI YA ASILIMIA 5.75 KWA TAHADHARI YA HATARI ZA KIMATAIFA

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kuendelea kubakiza kiwango chake cha riba ya msingi ya ukopeshaji (benchmark lending rate) katika asilimia 5.75 kwa robo ya pili ya mwaka huu, ikionesha tahadhari kufuatia kuongezeka kwa sintofahamu katika uchumi wa dunia.

Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha hivi karibuni cha Kamati ya Sera ya Fedha (MPC), ambapo watunga sera walitathmini hatari zinazotokana na mazingira ya kimataifa dhidi ya uimara wa uchumi wa ndani.

Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Yamungu Kayandabila, alisema hatua hiyo inalenga kusawazisha kati ya kukuza uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei.

“Haikuwa uamuzi rahisi,” alisema, akieleza kuwa mvutano wa kisiasa unaoendelea katika Mashariki ya Kati umeanza kuathiri mwenendo wa masoko ya dunia.

Alifafanua kuwa mvutano huo umevuruga minyororo ya usambazaji wa bidhaa na kuchangia kupanda kwa bei, hususan mafuta ambayo sasa yamevuka dola za Marekani 100 kwa pipa, juu ya makadirio ya awali.

Katika hatua nyingine, MPC ilitangaza kupunguza wigo wa riba (interest rate corridor) unaozunguka kiwango cha CBR kutoka pointi 200 hadi 150 za msingi (basis points), hatua inayoweka kiwango cha riba ya siku saba kati ya benki katika viwango vya asilimia 4.25 hadi 7.25.

Kwa mujibu wa Dkt. Kayandabila, hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa sera ya fedha, huku ikidumisha uthabiti wa bei na kusaidia ukuaji wa uchumi.

Licha ya changamoto za kimataifa, BoT imeeleza kuwa uchumi wa ndani unaendelea kuonesha uimara.

Katika robo ya kwanza ya mwaka, uchumi ulikua kwa asilimia 6.2 Tanzania Bara na asilimia 6.7 Zanzibar, ukichochewa na sekta za ujenzi, kilimo, utalii na huduma za kifedha.

Kwa robo ya pili, ukuaji unatarajiwa kufikia asilimia 6.1 kwa Tanzania Bara na asilimia 6.6 Zanzibar, ingawa hatari za nje zinaweza kuathiri mwenendo huo endapo zitaongezeka.

Kwa upande wa mfumuko wa bei, umeendelea kubaki ndani ya lengo la BoT la asilimia tatu hadi tano. Kwa wastani, ulikuwa asilimia 3.3 Tanzania Bara na asilimia 4.5 Zanzibar, hali iliyochangiwa na utulivu wa bei za chakula pamoja na kiwango cha ubadilishaji fedha.

Hata hivyo, Benki Kuu imeonya kuwa ongezeko la gharama za nishati na usafirishaji linaweza kuongeza shinikizo la mfumuko wa bei katika miezi ijayo.

Katika sekta ya benki, hali imeendelea kuwa imara ambapo kiwango cha mikopo chechefu kimeshuka hadi asilimia 2.9, chini ya kiwango kinachokubalika kisheria, huku benki zikiendelea kuwa na mtaji wa kutosha na ukwasi wa kuridhisha.

Kwa upande wa sekta ya nje, nakisi ya akaunti ya sasa imepungua hadi asilimia 2.2 ya Pato la Taifa (GDP), ikichangiwa na kuongezeka kwa mauzo ya nje ya dhahabu, mazao ya kilimo na huduma za utalii.

Zanzibar nayo imeendelea kufanya vizuri, ikirekodi ziada ya akaunti ya sasa kutokana na mapato ya utalii.

Aidha, akiba ya fedha za kigeni imefikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 6.2, kiwango kinachoweza kugharamia uagizaji wa bidhaa kwa karibu miezi mitano, juu ya viwango vya kikanda.

Kwa upande wa mapato ya serikali, makusanyo ya kodi yamevuka malengo kutokana na kuimarika kwa usimamizi na utii wa walipakodi, huku matumizi ya serikali yakiendelea kubaki ndani ya mipaka ya rasilimali zilizopo.

Hata hivyo, MPC imeonya kuwa bado kuna hatari zinazoikabili uchumi.

“Tishio kubwa kwa matarajio ya uchumi ni mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati. Endapo utaongezeka, unaweza kuongeza mfumuko wa bei na kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi duniani na nchini,” alisisitiza Dkt. Kayandabila.








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad