Na Elimu ya Afya kwa Umma
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imewahimiza Watanzania kurejea katika matumizi ya vyakula vya asili kama sehemu muhimu ya kujenga afya bora, kuzuia magonjwa, na kusaidia matibabu kwa njia salama na endelevu.
Akizungumza jijini Dodoma katika Mkutano wa Waziri wa Afya na wataalam wa tiba asili, Mkurugenzi wa Huduma za Uhamasishaji wa Afya (Elimu ya Afya kwa Umma), Dkt. Rahma Ahmed Hingora, amesema vyakula vya asili vina mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya mwili na vinaweza kutumika kama sehemu ya kinga na tiba iwapo vitatumika kwa usahihi.
“Tunapaswa kurudisha utamaduni wa kula vyakula vya asili kama maboga, ubuyu na vyakula vingine vinavyopatikana katika mazingira yetu. Hivi ni vyakula vyenye virutubishi muhimu vinavyosaidia kuimarisha kinga ya mwili na afya kwa ujumla,” amesema Dkt. Hingora.
Amebainisha kuwa kumekuwa na mabadiliko ya mtindo wa maisha ambapo jamii imekuwa ikipuuza vyakula vya asili na kuelekea zaidi katika matumizi ya vyakula vilivyosindikwa, ambavyo mara nyingi hupoteza virutubisho muhimu na vinaweza kuongeza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza.
“Ni muhimu kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya kemikali na virutubisho bandia kwenye vyakula. Turejee kula vyakula katika hali yake ya asili. Kula chakula kama dawa, na usisubiri kula dawa kama chakula,” amesisitiza.
Aidha, Dkt. Hingora amesema Serikali itaendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya afya kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari, majukwaa ya kidijitali, pamoja na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, ili kuhakikisha jamii inapata uelewa sahihi kuhusu lishe bora na matumizi salama ya vyakula vya asili.
Katika mkutano huo, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, alisisitiza umuhimu wa kuunganisha maarifa ya tiba asili na tiba ya kisasa, huku akihimiza wataalam kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa jamii kuhusu mchango wa vyakula vya asili katika afya.
Serikali inaamini kuwa matumizi sahihi ya vyakula vya asili yanaweza kusaidia kupunguza hatari ya magonjwa, kuimarisha kinga ya mwili, na kuchangia ustawi wa afya ya wananchi kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment