Waziri wa Fedha wa Tanzania, Khamis Mussa Omar umza wakati wa mkutano huo uliofanyika leo Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam wakati kujadiliana juu ya uwekezaji na biashara yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 7.8 nchini Tanzania katika mkutano wa Bodi ya taasisi hiyo.
Na Mwandishi Wetu
AFRICAN Trade & Investment Development Insurance (ATIDI) imejadili uwekezaji na biashara yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 7.8 nchini Tanzania katika mkutano wa Bodi ya taasisi hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam, hatua inayolenga kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wenye mitaji mikubwa.
Akizungumza wakati wa mkutano huo uliofanyika leo Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha wa Tanzania, Khamis Mussa Omar amesema kufungua uwezo kamili wa uchumi wa Tanzania kunahitaji ushirikiano imara unaoweza kuhamasisha mitaji mikubwa ya uwekezaji.
Amesema ATIDI imekuwa mshirika muhimu katika kupunguza hatari za uwekezaji, hali inayosaidia kuvutia mitaji ya sekta binafsi na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Pembeni mwa mkutano huo, uongozi wa ATIDI ulikutana na maafisa wa serikali, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo pamoja na wadau wa sekta binafsi kujadili namna ya kuimarisha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Majadiliano hayo yaliambatana na warsha ya wadau wa ngazi ya juu iliyopewa jina la “Kuimarisha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Tanzania,” iliyolenga kuboresha mfumo wa kifedha na kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Washiriki wa mkutano huo walisisitiza umuhimu wa kupata suluhisho la pamoja katika kuongeza mtiririko wa mitaji kutoka sekta binafsi ili kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa gharama nafuu katika sekta muhimu za uchumi na kukuza biashara za kikanda.
Tanzania ina nafasi ya kipekee katika historia ya ATIDI ikiwa ni miongoni mwa nchi wanachama waanzilishi tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2001 kwa msaada wa Common Market for Eastern and Southern Africa (COMESA) na World Bank.
Kwa mujibu wa takwimu za taasisi hiyo, kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita ATIDI imewezesha uwekezaji na biashara za mipakani barani Afrika zenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 93 kupitia huduma zake za bima ya mikopo ya biashara na uwekezaji.
Nchini Tanzania pekee, taasisi hiyo imesaidia zaidi ya sera 200 za bima, hatua iliyowezesha biashara na uwekezaji wenye thamani ya dola bilioni 7.8 huku kiwango cha hatari kinachodhibitiwa kikiwa karibu dola bilioni 1.8.
Uwekezaji huo umeelekezwa katika sekta muhimu za maendeleo ikiwemo miundombinu, nishati, mawasiliano na makazi nafuu.
Miongoni mwa miradi mikubwa iliyoungwa mkono ni reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) Tanzania ambayo imeendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ATIDI, Manuel Moses amesema changamoto kubwa kwa Afrika si ukosefu wa fursa bali ni hatari zinazohusiana na uwekezaji.
Naye Mtaalamu Mkazi wa Bima wa ATIDI, Tusekile Kibonde amesema taasisi hiyo inaendelea kutoa suluhisho za kupunguza hatari zinazowezesha upatikanaji wa fedha kwa miradi mikubwa barani Afrika huku akibainisha kuwa ushirikiano huo unasaidia kubadilisha fursa za uwekezaji kuwa ukuaji endelevu wa uchumi.

No comments:
Post a Comment