Na Khadija Kalili, Kibaha
MKOA wa Pwani unaungana na Mikoa mingine nchini kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi 2026 maadhimisho hayo Kimkoa yatafanyika katika Uwanja wa Ujamaa wa Ujamaa, Kata ya Umwe, Tarafa ya Ikwiriri, Halmashauri ya Mji Rufiji.
Mratibu wa maadhimisho hayo Mkoa wa Pwani, Roseline Kimaro, amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.
Kimaro amesema kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inasema , “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi Dira 2050,” ambayo inalenga kusisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na upatikanaji wa haki kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu ya taifa.
Amesema kuwa kuwa lengo kuu la maadhimisho hayo ni kutambua, kuthamini na kusherehekea mchango mkubwa wa wanawake katika nyanja mbalimbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi, sambamba na kuhimiza jamii kuendelea kusimamia na kulinda haki za wanawake na wasichana.
“Maadhimisho haya pia ni jukwaa la kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na kuhamasisha ushiriki sawa wa wanawake katika fursa za maendeleo,” amesema Kimaro.
Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa, maadhimisho yataanza rasmi Machi 1 hadi Machi 7 kwa kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii, zikiwemo utoaji wa elimu kwa umma, kampeni za uhamasishaji kuhusu usawa wa kijinsia, pamoja na shughuli za kijamii zitakazowahusisha wanawake na wadau wa maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.
Kimaro ameongeza kwa kusema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri ili kuhakikisha kilele cha maadhimisho hayo kinafanyika kwa mafanikio na kufikisha ujumbe kwa jamii kwa upana zaidi.
Aidha amevitaka vyombo vya habari, taasisi mbalimbali na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho hayo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuinua hadhi na kulinda haki za wanawake na wasichana katika Mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla.



No comments:
Post a Comment