MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeonesha mshikamano na jamii kwa kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu. Vituo vilivyonufaika na msaada huo ni Umra Orphanage Center kilichopo Magomeni Mikumi na Mother of Mercy Children’s Home kilichopo Madale, Dar es Salaam. Hatua hiyo pia ni sehemu ya kuwatakia kheri ya Sikukuu ya Eid el Fitri na Pasaka.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo Machi 29, 2025, jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, aliwapongeza walezi wa watoto kwa kazi kubwa wanayofanya. Alisisitiza kuwa jukumu la kuwasaidia watoto ni la jamii nzima na serikali inaendelea kuhakikisha inawafikia wahitaji kupitia michango ya walipa kodi.
"Zoezi hili tunalifanya katika mikoa yote 26 nchini kwani tumebaini maeneo yenye uhitaji ni mengi hivyo hii ni kama njia ya kurudisha kwa jamii..,TRA ni sehemu ya jamii na inaguswa na changamoto za watoto hawa, ndiyo maana tupo hapa leo,” alisema Mwenda.
Aliendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuchangia maendeleo ya nchi kwa kulipa kodi, akieleza kuwa mapato yanayokusanywa yanasaidia serikali kutoa huduma muhimu kwa jamii. Katika hatua ya kuonesha mchango wake binafsi, Kamishna Mwenda aliahidi kutoa shilingi milioni nne kusaidia upatikanaji wa bima ya afya kwa watoto wa Umra Orphanage Center. Pia aliwatia moyo watoto wa kituo hicho kusoma kwa bidii ili kutimiza malengo yao.
Katika tukio jingine, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano TRA, Richard Kayombo, pamoja na Naibu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Nahoda Nahoda, walikabidhi msaada kwa kituo cha Mother of Mercy Children’s Home.
Kayombo aliwatia moyo watoto wa kituo hicho na kuwaahidi kuwa TRA itaendelea kushirikiana nao. Alibainisha kuwa TRA inatambua umuhimu wa kusaidia makundi yenye uhitaji na itaendelea kutoa mchango wake kwa jamii.
Kwa upande wao, Muasisi wa Umra Orphanage Center, Rahma Kishumba, na msimamizi wa Mother of Mercy Children’s Home, sister Christina Christopher, waliishukuru TRA kwa msaada huo, wakisema umewapa faraja na kuwahakikishia watoto wao usaidizi katika maandalizi ya sikukuu.
Msaada huu unaonesha dhamira ya TRA katika kusaidia jamii na kuhakikisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanapata mahitaji ya msingi, hasa katika kipindi cha sikukuu.

No comments:
Post a Comment