HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 12, 2024

CMSA YAZINDUA MPANGO UWEKEZAJI WA PAMOJA UNAOHUSISHA MIFUKO MITANO

 

 

*Yasisitiza kuendeleza na kusimamia Masoko ya mitaji nchini


Na Mwandishi Wetu Michuzi TV

MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesisitiza kuwa ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.

Imetoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo CPA Nicodemus Mkama wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa uwekezaji wa pamoja wa Kampuni ya iTRUST Finance Limited unaojumuisha mifuko mitano ya uwekezaji wa pamoja uitwao iCASH Fund,iGROWTH FUND,iINCOME FUND,iSAVE FUND NA IMAAN FUND.

"Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) itaendelea kutekeleza na kusimamia utekelezaji wa mikakati yenye lengo la kuchagiza maendeleo ya masoko ya mitaji na hivyo kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu."

Kuhusu uzinduzi wa mpango wa uwekezaji pamoja kwa kampuni hizo CPA Mkama amesema Oktoba 11 Oktoba 2024, CMSA) iliidhinisha nyaraka za matarajio na mikataba ya uendeshaji wa mifuko mitano ua uwekezaji wa pamoja ya kampuni ya iTrust Finance Limited.

Ameongeza idhini ilitolewa na CMSA baada ya iTrust Finance Limited kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Kanuni za Masoko ya Mitaji na Dhamana za Uanzishaji na Uendeshaji wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.

"Mifuko hii imekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja. Aidha, iTrust Finance Limited inakuwa kampuni ya kwanza nchini Tanzania kuzindua Mifuko Mitano (5) ya uwekezaji kwa wakati mmoja."

Amefafanua mifuko hiyo inaendeshwa na kampuni ya iTrust Finance Limited, ambayo ina jukumu la kuendesha na kusimamia mifuko (Fund Manager) na Benki ya NBC ambayo ina jukumu la kutunza Dhamana za Mifuko (Custodian Bank).

CPA Mkama amesema lengo kuu la mifuko hiyo ni kuwawezesha wawekezaji wadogo, wa kati, na wakubwa kuunganisha nguvu zao na kuwekeza kwa pamoja ili kunufaika na fursa zinazopatikana katika sekta ya fedha, hususan masoko ya mitaji.

Aidha, malengo mahsusi ya mifuko hiyo ni kuwawezesha watanzania wa kada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake, makundi maalum, taasisi na mifuko ya hifadhi ya jamii kunufaika na uwekezaji unaosimamiwa na wataalamu waliopewa leseni ya kutoa huduma katika masoko ya mitaji; kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza; na kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za uchumi, na hivyo kuongeza vipato vyao.

"Kuanzishwa kwa mifuko hii ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi wengi zaidi mijini na vijijini na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

" Utekelezaji wa azma hii umeainishwa katika Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha 2023-2028 wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha ikiwa ni pamoja na masoko ya mitaji."

Amesema mauzo ya awali ya vipande vya mifuko hii yanafunguliwa leo Novemba 12, 2024, ambapo kampuni ya iTrust Finance Limited inatarajia kukusanya jumla ya Sh. bilioni 37 na kwamba kwa mujibu wa Sera na miongozo ya uwekezaji wa mifuko hiyo fedha zitakazopatikana kutoka kwa wawekezaji zitawekezwa katika masoko ya fedha na masoko ya mitaji.

Ameongeza ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa, Hatifungani za Serikali, Hatifungani za Kampuni na Dhamana za Serikali za muda mfupi.

Amesema kuwa lengo la uwekezaji wa aina hiyo ni kuifanya mifuko kuwa na ukwasi unaotosha ili kukidhi mahitaji ya fedha za wawekezaji pindi mahitaji yanapotokea. Aidha, kwa upande wa mfuko wa Imaan, fedha zitakazopatikana zitawekezwa kwenye bidhaa za masoko ya mitaji zinazozingatia misingi ya Shariah, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika hatifungani za Sukuk.

Aidha amesema uwekezaji katika mifuko hiyo una manufaa mbalimbali katika ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi hapa nchini ikiwemo ya kuchangia katika utekelezaji wa Sera ya Serikali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kuwezesha makundi mbalimbali ya jamii.

 




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad