HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 25, 2024

THBUB YATHIBITISHA TUHUMA ZA UKIUKWAJI HAKI ZA BINADAMU MGODI WA NORTH MARA SIO ZA KWELI


Na Mwandishi wetu.

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini (THBUB), imebaini kuwa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu zilizotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Mining Watch la nchini Canada dhidi ya mgodi wa dhahabu wa North Mara, wakati wa mchakato wa upanuzi wa shughuli za mgodi sio za kweli.

Ripoti ya Tume hiyo iloyotolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wake, (Jaji Mstaafu) Mathew Mwaimu, imeeleza kuwa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, ulifuata sheria na taratibu stahiki katika kutwaa ardhi yenye ukubwa wa ekari 652 katika kijiji cha Komarera kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za uchimbaji.

Vijiji Vilivyodaiwa wakazi wake walifanyiwa vitendo vya ukiukwaji haki za Binadamu ni Komarera na Kewanja vilivyopo wilayani Tarime mkoani Mara.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa baada ya uchunguzi wa tuhuma hizo, Tume ilibaini kuwa uthamini na utwaaji wa ardhi kwenye eneo husika ulifuata taratibu za Nchi na ulifanyika kwa uwazi na ushirikishwaji wa pande zote, na wananchi ambao maeneo yao yalitwaliwa walilipwa fidia stahiki.

THBUB ilifanya uchunguzi kuhusu malalamiko hayo dhidi ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga, yaliyodai kutozingatia utaratibu wa utwaaji wa ardhi mwaka 2021 na 2022, kwa kuwaondoa wananchi katika ardhi yao kwa kutumia nguvu, vitisho, ukatili na udhalilishaji.

Kabla ya kuanza uchunguzi wa tuhuma hizi, mwezi April 2024, Barrick ilipokea barua ya malalamiko yaliyotolewa na shirika hilo lisilo la Kiserikali la Mining Watch la Canada, kutoka kwa Afisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Beatriz Balbin, ili kupata ufafanuzi wa tuhuma hizo na ndipo THBUB ilianza pia kuzifanyia kazi ili kubaini kama zina ukweli.

Uongozi wa Barrick umetolea ufafanuzi wa tuhuma hizo kwa kufafanua kuwa hapakuwepo na ukiukwaji wowote wa haki za binadamu katika kutekeleza zoezi hilo kwa kuwa ulifuata mchakato wote kwa mujibu wa maelekezo ya sheria za nchi ambao ulifanyika kwa uwazi na ulikuwa shirikishi kwa wananchi wote waliohamishwa sambamba na kuhusisha taasisi mbalimbali za serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad