HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 11, 2024

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA KITUO CHA POLISI DARAJA A MTUMBA DODOMA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiweka jiwe la msingi la Ufunguzi wa Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba mkoani Dodoma tarehe 11 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa hafla ya kufungua Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba na Kukabidhi Magari 21 kwa Jeshi la Polisi iliyofanyika eneo la Mtumba Mkoani Dodoma  tarehe 11 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua Gwaride la Jeshi la Polisi mara baada ya kuwasili eneo la Mtumba Mkoani Dodoma kufungua Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba na Kukabidhi Magari 21 kwa Jeshi la Polisi. Tarehe 11 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba mkoani Dodoma tarehe 11 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kuhusu mfumo wa kidijitali wa ufunguaji kesi uliopo katika Kituo cha Polisi Mtumba wakati wa akikagua kituo hicho katika hafla ya  Ufunguzi wa Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba mkoani Dodoma tarehe 11 Mei 2024. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kufuata taratibu, kuzingatia sheria ya Jeshi la Polisi na kanuni za Polisi katika kufanya kazi za Kipolisi ikiwemo kukamata, kufanya upekuzi, kushikilia, kupeleleza watuhumiwa pamoja na kuwahoji mashahidi na watuhumiwa.


Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa hafla ya kufungua Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba na Kukabidhi Magari 21 kwa Jeshi la Polisi, hafla iliyofanyika eneo la Mtumba Mkoani Dodoma. Amesema Maadili mema, nidhamu kazini na uwajibikaji ni nguzo muhimu kwa Jeshi la Polisi katika kusimamia sheria. Makamu wa Rais amelipongeza Jeshi la Polisi pamoja na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama kwa kuendelea kuimarisha Amani na usalama hapa nchini.


Aidha Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Jeshi la Polisi kubadilika kwa haraka ili kuweza kukabiliana na mbinu mpya za uhalifu kwa kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake. Amewasihi kujielekeza zaidi katika kubuni na kutumia mifumo ya TEHAMA na kuhakikisha Askari na Makamanda wanapata mafunzo ya mara kwa mara kwenye maeneo ya intelijensia, usalama na uhalifu wa kimtandao,akili mnemba na matumizi ya roboti pamoja na kuunganisha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na Mikoa, Wilaya, Vikosi, Vitengo na Vituo vyote vya Polisi nchini ili kurahisisha mawasiliano.


Vilevile Makamu wa Rais amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuangalia upya mfumo mzima wa utoaji leseni, ukaguzi wa magari, matumizi ya teknolojia hususan kamera za barabarani na matumizi ya Body-cam jackets  zitakazoonesha mazungumzo baina ya askari na madereva ili kudhibiti rushwa barabarani,kuimarisha weledi na uthabiti wa vyombo vya moto hali itakayosaidia katika kudhibiti ajali za barabarani.


Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni muhimu kwa Jeshi la Polisi kujenga uhusiano mzuri kati yake na wananchi ili liweze kufanikiwa kubaini, kuzuia na kudhibiti uhalifu wa aina zote. Pia ameitaka jamii kuheshimu sheria na taratibu za Jeshi la Polisi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao. Amesema Jitihada zinazofanyika kupitia dhana ya Polisi Jamii ni budi ziendelezwe.


Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kufanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai yaliyo ndani ya uwezo wake  ikiwemo kuimarisha Madawati ya Malalamiko ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi kwa kuyapatia watumishi wa kutosha wenye weledi kwenye masuala ya uchunguzi ili kuendelea kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi nchini.


Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amesema Jeshi la Polisi limeendelea kukuza matumizi mbalimbali ya mifumo ya TEHAMA ikiwa ni utekelezaji maelekezo ya Mheshimiwa Rais katika kuleta ufanisi, uwazi na uharaka wa kazi za Kipolisi kwa lengo la kuharakisha masuala yote ya haki jinai na kuhakikisha yanatendeka kwa tija.


Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura amesema Jeshi la Polisi linatambua deni kubwa walilonalo kwa Serikali na Wananchi hivyo litazidisha utendaji wenye nidhamu ya hali ya juu, haki, uadilifu na kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi ni huduma sahihi na zinazotakiwa. 


Ameongeza kwamba ujenzi wa Vituo hivyo vya kisasa vya Polisi utawezesha kutafsiri madhumuni halisi ya kuwepo kwa Jeshi la Polisi kwa kuwa majengo hayo ni rafiki hata kwa watendaji katika kutimiza wajibu wao.  


Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

11 Mei 2024

Dodoma.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad