HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, February 25, 2024

VIJANA JKT WAPONGEZWA KWA KUONESHA UZALENDO MSOMERA

 VIJANA  wanaoshiriki kwenye kazi mbalimbali za ujenzi katika Kijiji cha Msomera wamepongezwa kutokana na kufanya kazi kwa kujituma na kuonesha uzalendo kwa taifa ili kufanikisha mpango wa serikali wa kuwahamisha wananchi kwa hiyari kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.


Akizungumza mara baada ya kamati ndogo ya ulinzi na usalama kutembelea eneo hilo Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kamishna wa Polisi Charles Mkumbo amesema vijana hao ambao wanashiriki katika kazi hizo wameonesha uzalendo mkubwa katika kutimiza majukumu yao kwa maslahi ya taifa.

Amesema zoezi la ujenzi wa nyumba linalofanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kupitia SUMA-JKT limeonesha mafanikio makubwa ambapo kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo ujenzi wa nyumba 2559 katika Kijiji cha Msomera linatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi ujao.


Mapema Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mheshimiwa Albert Msando amesema pamoja na jeshi hilo kufanya kazi vizuri changamoto kubwa kwa sasa ni kwa baadhi ya Wizara za kisekta kutokuwa na kasi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo licha ya fedha kutolewa na serikali.


Ametoa wito kwa watendaji wote wa serikali katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni kufanya kazi usiku na mchana ili kuweza kukamilisha miradi yote kwa wakati huku akiipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuendelea kuhamasisha wananchi kuhama kwa hiyari na kuwahamisha.

Akielezea kuhusiana na zoezi la uhamasishaji na uandikishaji linavyoendelea Kaimu Meneja wa Mradi wa zoezi hilo Flora Assey amesema kwa sasa kazi inaendelea kwa kasi kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Bi Flora amesema kwamba Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kuhamisha wananchi kutoka ndani ya Hifadhi kadri nyumba na miundombinu mengine itakavyokuwa inakamilika.

Serikali ya Tanzania imeamua kuhamisha wananchi kwa hiyari kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kuwawezesha wananchi hao kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi tofauti na ilivyo sasa ikiwa ni pamoja na kulinda Hifadhi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad