Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa pongezi na shukurani kwa Vyombo vyote vya Habari na Wanahabari kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhabarisha umma juu ya huduma zinazotolewa na Jeshi hili hapa nchini. Mmekuwa kiungo kikubwa na daraja la mawasiliano baina yetu
Jeshi linawajulisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2023, lilikabiliana na matukio ya majanga ya moto, Ajali za barabarani, uokoaji nchi kavu na majini. Pia tumeendelea kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya majanga, kutoa elimu kwa umma pamoja na kufanya uchunguzi wa majanga mbalimbali.
Katika kipindi cha Januari hadi Disemba, 2023 tulikabiliana na matukio ya Moto 2,076 ambayo yalisababisha vifo vya Watu 38 na Majeruhi 146, ukilinganisha na matukio hayo katika kipindi cha mwaka uliopita 2022, ambapo kulikuwa na matukio ya Moto 1,854 vifo vya Watu 32 na Majeruhi 66
Tulifanikiwa kutoa huduma za Uokoaji katika Maeneo 1,195, matukio hayo yalisababisha Vifo 684 na Majeruhi 1,465, ukilinganisha na matukio ya Uokoaji 567, vifo na Majeruhi 1,010 Mwaka uliopita 2022. Aidha tunatoa pole kwa wote waliopoteza ndugu na jamaa zao katika majanga hayo
Jumla ya maeneo 12,382 yalipatiwa elimu moja kwa moja na Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ukilinganisha na maeneo 7,511 yaliyofikiwa mwaka 2022, kupitia Vyombo vya Habari tumefanya vipindi 728, ikiwa vipindi 606 vya Redio na 122 vya Luninga, ukilinganisha na vipindi 602 vilivyofanyika mwaka 2022 ikiwa Redio 467 na Luninga 135.
Katika ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto tulifanikiwa kuyafikia maeneo 61,424 ambayo yalifanyiwa ukaguzi ukilinganisha na maeneo 42,858 mwaka 2022, michoro ya ramani za majengo 2,431 zilipitishwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kupata ushauri wa kitaalam ukilinganisha na michoro ya ramani za majengo 297 mwaka uliopita 2022.
Tunauhakikishia umma tutaendelea kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto, kutoa elimu kwa umma, kushirikiana na Halmashauri za Miji na Majiji ili kuhakikisha tunapanga Miji yetu ili iwe salama wakati wa Majanga na kuliwezesha Jeshi kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati bila kuwa na vikwazo vyovyote.
Tunatoa rai kwa Wananchi wote kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria au tukio la Moto au ajali ya barabarani ikiwa kuna uhitaji wa huduma ya Uokoaji, wasisite kupiga namba yetu ya dharura ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji 114 ambayo ni bure kabisa.
Aidha, Tunapenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuliongezea nguvu kazi, kupandisha vyeo vya Maafisa na Askari na kuliwezesha fedha za miradi ya maendeleo ili kuongeza na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma zake kwa Wananchi.
Zimamoto na Uokoaji “Okoa Maisha na Mali Piga namba 114.”
Wednesday, January 10, 2024
Home
Unlabelled
JESHI LA ZIMAMOTO LAELEZA MAFANIKIO YA UTOAJI HUDUMA KWA KIPINDI CHA MWAKA 2023
JESHI LA ZIMAMOTO LAELEZA MAFANIKIO YA UTOAJI HUDUMA KWA KIPINDI CHA MWAKA 2023
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment