HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 15, 2024

WANAWAKE WATAKIWA KUSOMEA UBAHARIA KUKUZA UCHUMI

Mkuu wa chuo cha bahari Dar-es-salaam (DMI) dkt. Tumaini Gurumo akielezea kuhusiana na fani zinazosomeshwa katika chuo hicho alipotembelewa na waandishi wa habari katika maonesho ya 10 ya biashara yanayoendelea katika kituo cha biashara Nyamanzi Zanzibar.

Na Fauzia Mussa , Maelezo Zanzibar
MKUU wa chuo cha bahari Dar-es-salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo amewataka wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wao wakike kusomea fani za ubaharia ili kuweza kuzifikia fursa zitokanazo na uchumi wa buluu na kujiletea maendeleo.

Wito huo ameutoa wakati akifanya mahojiano na waandishi wa habari walipotembelea banda la chuo hicho katika maonesho ya 10 ya biashara yanayoendelea katika kituo cha biashara Nyamanzi Zanzibar.

Alisema ili kutekeleza dhana ya uchumi wa buluu kwa vitendo ipo haja kwa vijana kuendelea kujiunga na chuo hicho bila kujali jinsia ili kupata mafunzo yatakayowawezesha kuingia katika utekelezaji wa dhana hiyo,kwani bila rasilimali watu wenye weledi lengo la uchumi wa buluu halitafikiwa.

Amesema dhana ya uchumi wa buluu imeenda kuongeza ari na kasi kwa wazanzibar kujiunga kwa wingi siku hadi siku katika chuo hicho, na kusema kuwa kutokana na mwamko huo chuo kina mpango wa kuanzisha tawi kisiwani pemba ili kuhakikisha Tanzania nzima inaunufaika na huduma za chuo hicho.

“mwamko wa wazanzibar kujiunga na chuo hichi ni mkubwa sana kwasasa tuna mpango wa kutafuta eneo pemba ili tuweke tawi la chuo chetu kwa lengo la kusogeza huduma kisiwani humo,tusipofanya hivyo tutakua tunakaribisha wageni kujakufanya kazi katika maeneo yetu na kupelekea uchumi tuliokusudia urudi nyumbani kwenda kwa wageni” alifahamisha dkt. Tumaini

Amesema ili nchi ipate maendeleo si vyema kuwawekea wasichana mipaka ya kusomea fani fulani kwani nafasi za ajira zilizopo maelini hazichagui jinsia .

Alieleza kuwa kwa sasa mwamko wa wanawake kusomea fani hiyo ni mdogo hivyo alitumia fursa hiyo kushajihisha wazazi na walezi kuwapa nafasi wasichana kusomea fani hiyo kwa maslahi yao binafsi na taifa kwa ujumla.

“tuwaache vijana wasomee fani wanazozipenda ,hakuna kitu kizuri kama mtu kufanya kazi anayoipenda ,wanawake wana haki ya kusomea ubaharia pia na hata sheria zinatoa haki sawa na maslahi kati ya wanawake na wanaume”alifahamisha mkuu huyo

Amesema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho wazanzibar kwa ujumla wamekuwa na mwamko mkubwa wa kusomea fani ya ubaharia chuoni hapo licha ya kuwa chuo chenyewe kipo Dar-es-salaam .

Akizungumzia mafanikio ya miaka 60 ya mampinduzi katika chuo hicho dkt. Tumaini alisema chuo kimefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka wanafunzi 12 kwa mwaka 1978 hadi kufikia kuwa na zaidi ya wanawafunzi elfu 4 kwa mwaka 2023-2024.

Aidha alifahamisha kuwa chuo hicho kimekua kikitengeneza rasilimali watu zinazoweza kunufaisha ukanda mzima wa Tanzania na nje ya Tanzania pamoja na kufanikiwa kufanya tafiti za bahari ili kuweza kufanya vizuri katika dhana ya uchumi wa buluu.

“Ili tuweze kuanya vizuri katika uchumi wa buluu ni lazima tufanye tafiti kuweza kutathmini ni upande gani tuende zaidi ,kama ni uvuvi wa aina gani utaleta tija zaidi” alisema dkt. Tumaini

Licha ya mafanikio hayo dkt. Tumaini alisema kuwa chuo kinakabiliwa na uhaba wa walimu mabaharia wenye sifa zinazokubalika kulingana na uhitaji wa wingi wa wanafunzi wanaongezeka kusajiliwa siku hadi siku.

Vilevile wanafunzi wamekuwa wakikosa nafasi za kushiriki mafunzo kivitendo katika meli zinazosafiri kutoka nchi moja kwenda nyengine,hivyo aliziomba taasisi za usimamizi wa meli za serikali na binafsi kusaidia wanafunzi wengi kupata nafasi za mafunzo melini ili kurahisisha upatikanaji wa ajira za nje na ndani ya nchi kwa vijana hao.

Awali alifahamisha kuwa lengo la kushiriki katika maonesho hayo ni kutangaza shuguli zinazofanya na chuo hicho ambapo alisema ni pamoja na kutoa elimu na mafunzo ya mabaharia na masuala yanayohusiana na bahari kama uchimbaji wa gesi,utunzaji wa mzingira na usalama baharini.

MAELEZO YA PICHA

PICHA NO.01:- Mkuu wa chuo cha bahari Dar-es-salaam (DMI) dkt. Tumaini Gurumo akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na fursa zinazopatikana katika chuo hicho walipotembelea banda la DMI katika maonesho ya 10 ya biashara yanayoendelea katika kituo cha biashara Nyamanzi Zanzibar.

PICHA NO.02:- Mkuu wa chuo cha bahari Dar-es-salaam (DMI) dkt. Tumaini Gurumo akielezea kuhusiana na fani zinazosomeshwa katika chuo hicho alipotembelewa na waandishi wa habari katika maonesho ya 10 ya biashara yanayoendelea katika kituo cha biashara Nyamanzi Zanzibar.

PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad