HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 9, 2023

TAPSHA KUMPONGEZA RAIS DKT. SAMIA

Na Mwandishi Wetu
UMOJA wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (TAPSHA), Jiji la Dar es Salaam, umeazimia kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa anavyowezesha uboreshaji wa miundombinu katika shule zote nchini.

TAPSHA umetolea mfano maeneo yaliyoboreshwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya kupitia mradi wa BOOST kila kona nchini, vyoo vya kisasa vya wanafunzi, ukarabati wa vyumba vya madarasa, ununuzi na utengenezaji wa madawati, usambazaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupitia GPE LANES II na ugawaji wa vishikwambi kwa walimu.

Tamko hilo lilitolewa jijini Dar es Salaam mapema wiki hii na umoja huo kupitia risala iliyosomwa katika mkutano wao mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ambapo Mkutano huo ulibebwa na kauli mbiu isemayo; ‘Yamewezekana yasiyowezekana katika elimu nchini',

“Kauli hii inajidhihirisha wazi kwa jinsi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anavyowezesha uboreshaji wa miundombinu katika shule zetu kote nchini,” ilisema sehemu ya risala hiyo.

Umoja huo jijini humo, unaoundwa na walimu 309 kati ya hao walimu wakuu ni 139 wa shule za serikali na walimu 170 wa shule zisizo za serikali zilizopo jijini humo, ulitaja mafanikio ni kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano mwema miongoni mwa waliku wakuu na viongozi wao mbalimbali.

Mafanikio mengine ni kupungua kwa idadi ya wanafunzi wasiomudu KKK katika shule zao kutokana na maazimio waliyojiwekea katika mikutano iliyopita ya kuhakikisha wanapunguza wanafunzi wasiojua KKK.

Pia, imeelezwa kuwepo kwa ongezeko la ufaulu katika mitihani ya kitaifa, ambapo halmashauri hiyo inaongoza kwa miaka mitatu mfululizo, usimamizi mahiri wa miradi ya maendeleo inayoletwa katika shule, kusimamia shule kwa weledi na kupunguza migogoro mahali pa kazi na kuendelea kusimamia vizuri suala la lishe katika shule zao.

Pamoja na mafanikio hayo, umoja huo umebainisha kukakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa walimu katika baadhi ya shule mpya, huku shule nyingi zikikabiliwa na uchakavu wa majengo na upungufu wa madawati, ukosefu wa meza na viti vya walimu, kuchelewa kwa malipo ya nauli za likizo kwa walimu.

Mwenyekiti wa TAPSHA, Wilaya ya Ilala, wa upande wa shule za msingi za serikali, Godrick Rutayungururwa, alisema walikuwa na mkutano mkuu wa tano kuwapa mrejesho wa mkutano mkuu wa tano wa taifa uliofanyika Dodoma.

Alisema, pia walikuwa wakiweka maazimio ya kwao ya mwaka 2024 na kupeana taarifa za mwaka 2023, ambapo alisema wameweka azimio la kumpongeza, Rais Samia, kwa jitihada anazozifanya za kuhakikisha elimu nchini anaendelea kuipa kipaumbele kwa ajili ya watoto na kuhangaikia maslahi ya walimu.

Mwenyekiti wa TAPSHA, upande wa shule za msingi binafsi Jefta Chaulo, alisema wameazimia kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya elimu.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliwapongeza walimu wakuu wa shule za msingi za serikali na binafsi kwa ufaulu ambao katika kipindi cha miaka minne Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inaongoza kitaifa

“Hata mwaka huu ufaulu umeongezeka kwa kiwango kikubwa mpaka kupata zaidi ya asilimia 97.8", huku akiupongeza umoja huo, kwa usimamizi mzuri wa miradi inayoendelea kutekelezwa katika ngazi za chini.

“Ninawasihi kuna fedha nyingi ambazo Rais anazipeleka katika halmashauri za utekelezaji wa miradi kwa hiyo na nyie ndiyo wasimamizi, mkaisimamie vizuri na lazima itekelezwe kwa ubora unaotakiwa,” aliwasihi.

Mpogolo alieleza kuwa, walimu wana thamani kubwa kwao kutokana na mafanikio wanayoendelea kuyapata huku akitolea mfano wa Septemba, mwaka huu. "Wakati wa likizo tulikuwa na zoezi la ukusanyaji wa takwimu za wafanyabiashara katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lakini tuliwatumia walio hao hao wa jiji la Dar es Salaam kubaini wafanyabiashara ambao walikuwa hawana leseni, waliokuwa na leseni feki na vibali feki", alisema Mpogolo.

Aidha, aliwaomba waendelee kumuunga mkono Mkurgenzi wa jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura, kutokana na jitihada mbalimbali anazozifanya, huku akitolea ufafanuzi wa ongezeko la mapato katika halmashauri hiyo kutoka Sh. Bil. sita mpaka Bil. 10 kwa mwezi na ongezeko la kutoka katika makusanyo wanalolitegemea kutoka Sh. Bil. 89 kwenda hadi Sh. Bil.120.

“Ninawaomba waendelee kumuunga mkono mkurugenzi huyo kwa kuwa kitendo hicho kimesaidia kwenda kutengeneza viti na meza kwa shule za sekondari 17,600 na madawati kwa shule za msingi 20,000.

“Kikubwa cha kujivunia sisi viongozi wa jiji la Dar es Salaam, tulikuwa tunatengeneza meza na viti kwa Sh 135,000 hivi sasa tunatengeneza kwa Sh 80,000 kwa maana yake kwa idadi hiyo ya 17,000 tumeweza kuokoa Sh. Mil 800,” alisema.

Aliendelea kusema kuwa kwa upande wa madawati ya shule za msingi zamani walikuwa wakitengeneza kwa Sh. 150,000, hivi sasa wanatengeneza kwa sh. 110,000 kwa kila dawati, hivyo kuokoa Sh. 40,000 kwa madawati 20,000 wameweza kuokoa Sh. Mil 800, ambapo kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya hiyo, halmashauri kwa upande wa madawati, viti na meza imeokoa Sh. Bil 1.6.

Pia aliwaomba waendelee kumwombea Rais Samia kwa kuwa amefanya mambo makubwa katika wilaya hiyo, ikiwemo kuwapatia zaidi ya Sh. Bil 15 kwa ajili ya uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu Msingi, kugharamia elimu bure na mitihani, Ununuzi wa Vitabu vya kinda na ziada na kupelekea ufaulu kufikia 98.7%, huku akisisitiza kuwa Ilala inaazimia kuwa na watoto wote wanaoanza shule wanamaliza na kufaulu.







No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad